July 14, 2020

KATIBU MKUU KILIMO AKEMEA KASI NDOGO YA MKANDARASI UJENZI WA VIHENGE NFRA MAKAMBAKO

Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (wa kwanza kushoto) akikagua mradi wa ujenzi wa vihenge vya kisasa na maghala yanayojengwa katika Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kanda ya Makambako. Katika ziara hiyo Katibu Mkuu amesema amesikitishwa kuona kasi ndogo ya mkandarasi Feerum toka Poland.


Na Mwandishi Wetu


Wakala wa Ujenzi (TBA) wametakiwa kufanya kazi ya kumsimamia kwa karibu mkandarasi wa ujenzi wa vihenge vya kisasa na maghala akamilishe kazi mapema kabla ya mwisho wa mwaka huu ili nchi iweze kuongeza uwezo wa kuhifadhi mazao yake.
 
Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa vihenge vya kisasa (silos) sita (6) vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 na maghala mawili (2) yenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 katika kanda ya Makambako unaogharimu shilingi Bilioni 26.5 chini ya kampuni ya Feerum toka nchini Poland.

Maagizo hayo ya serikali yametolewa 12.07.2020 na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya alipofanya ziara katika ofisi za NFRA kanda ya Makambako mkoa wa Njombe ambapo ameeleza kusikitishwa kwake na kasi ndogo ya kampuni ya Feerum kutekeleza mradi huo “Ikifika Desemba 31 mwaka huu nitakuja hapa Makambako,nataka TBA mnikabidhi kazi yangu ya maghala na vihenge ikiwa imekamilika.Hatuwezi kukubali mradi huu ushindwe kukamilika wakati serikali imeshatoa fedha nyingi” alisema Kusaya Katibu Mkuu huyo alisema kuwa hajafurahishwa na kasi ndogo ya mkandarasi iliyofikia asimilia 58 licha ya muda wake wa mkataba kuongezeka.

Akiwa eneo la mradi Katibu Mkuu Kusaya ameagiza msimamizi wa mradi huo TBA kupitia Mhandisi Mkazi wake Pedon Mshobozi kupata mpango kazi wa mkandarasi kuuwakilisha wizarani ili apate kujua endapo maghala na vihenge vitakamilika.

Kusaya alisema mradi huo ni sehemu ya miradi ya kimkakati ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli hivyo hatopenda kuona mkandarasi mzembe anavumiliwa bali hatua za kisheria ikibidi zichukuliwe kwa mujibu wa mkataba kumwondosha.

“ Serikali imeweka lengo la kuongeza uwezo wa nchi kuhifadhi chakula na nafaka kutoka tani 250,000 za sasa hadi kufikia tani 501,000 mradi huu utakapokamilika nchini mwaka huu kwenye vituo nane NFRA” alisisitiza Kusaya.
 
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa NFRA kanda ya Makambako Frank Felix alisema katika msimu wa 2020/2021 wamepangiwa kununua tani 25,000 za mahindi na mpunga
toka kwa wakulima.

Hadi kufika sasa amesema wakala umenunua jumla ya tani 4.258.986 kati hizo tani 2,933.174 za mahindi na tani 1,325.782 za mpunga na ametoa wito kwa wakulima kupeleka mazao yao kwenye vituo ili yanunuliwe.
 
Akizungumzia akiba iliyopo kituoni hapo Frank alisema wakala katika maghala yake ya Makambako una akiba ya tani 11,896.63 za nafaka

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Kusaya ametoa onyo kali kwa mameneja wa NFRA kanda zote nane kuacha mara moja kufanya kazi kwa maslahi binafsi.

Amesema anazo taarifa kuwa baadhi ya watendaji hao wa serikali wanajihusisha kuhujumu mali kwa maslahi binasfi kinyume na taratibu na sheria za utumishi wa
umma.

“ Nachukia sana mtumishi anayetumia vibaya fedha za umma.Sina huruma na watumishi wa aina hii.Sitasita kuwafukuza kazi wabadhirifu “ alisema Kusaya.

Ameitaka menejimenti ya wakala wa hifadhi ya taifa ya chakula kujituma zaidi na kuweka mpango wa kuwezesha kujiendesha kibiashara ili kutumia nafasi ya maghala na
vihenge vipya kutunza mazao mengi zaidi ya sasa.

Katibu Mkuu huyo yupo kwenye ziara ya kukagua utendaji kazi wa taasisi na wakala chini ya wizara yake kwenye mikoa ya Njombe, Iringa na Mbeya

No comments:

Post a Comment

Pages