July 08, 2020

KIFAA CHA KUPANDA MBEGU CHAVUTIA WENGI KATIKA MAONESHO YA SABASABA

Zana za kilimo.

 
Na Tatu Mohamed

WAKULIMA sasa huenda wakapata urahisi wa kupanda mbegu za mazao yao ikiwa ni baada ya kubuniwa kwa kifaa kitakachowawezesha wao kupanda kwa urahisi na kiasi kikubwa.

Kifaa hicho kilichobuniwa na Gema Tarimo ambaye ni mwalimu wa fani ya agro mechanics katika chuo cha Ufundi stadi (Veta) - Kihonda kimelenga kurahisisha ufanyaji kazi wa wakulima na kuongeza uzalishaji wao.

Akizungumza katika banda la Mamlaka ya Ufundi stadi (Veta) Tarimo amesema alifikia uamuzi wa kubuni kifaa hicho ili kurahisisha upandaji wa mbegu kwa wakulima na kuwapunguzia gharama walizokuwa wakizitumia awali.

“Zamani ili waweze kupanda eneo kubwa ilikuwa ni lazima wawe na watendakazi wengi tofauti na sasa ambapo kutumia kifaa hiki mtu mmoja anaweza kukisukuma mwenyewe au kutumia ng’onge au punda katika kulazimisha shughuli,” amesema.

“Kutokana na hilo mtu anakuwa na uwezo wa kupanda hadi ekari 2 kwa siku moja tena kwa urefu sawa,”

Ameongeza kuwa ili mkulima aweze kununua kifaa hicho atauziwa kikiwa na sahani za ndani (plate) tatu ikiwa ni kwa ajili ya kupandia mbegu tofauti.

“Urefu wa kupanda mahindi hauwezi kuwa sawa na ule wa maharage au karanga kwa sababu ukiangali mahindi ni lazima upande walau kuanzia sentimita 30, maharage sentimita 10 hadi 20 unaweza kupnada ndiyo maana ni lazima ziwe sahani tofauti,” amesema Tarimo.

“Na jinsi ilivyotengenezwa mtu anapokuwa anasukuma kifaa hiki kikazunguka kila baada ya sentimita kadhaa kulingana na mbegu husika kitatema mbegu,” amesema.

Amefafanua kuwa, kifaa hicho kinatumika hasa kwa wale wanaolima mfumo wa ‘sesa’ na si wale wanaotumia matuta.

Amesema kifaa hicho hutumia hadi mwezi mmoja kuwa tayari kwa matumizi na kinauzwa kwa Sh 600,000.

No comments:

Post a Comment

Pages