July 16, 2020

Membe atangaza rasmi kujiunga na ACT- Wazalendo

 Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika Serikali ya awamu ya nne, Bernard Membe, akizungumza katika mkutano wa kutambulishwa kwa wanachama wa Chama  cha ACT-Wazalendo baada uya kujiunga rasmi na chama hicho. (Picha na ACT-Wazalendo).
 Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalimu Seif Sharif Hamad, akiteta jambo na mwanachama mpya wa chama hicho, Bernard Membe.


Na Janeth Jovin

ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Nje katika Serikali ya awamu ya nne, Bernard Membe, leo ametangaza rasmi kujiunga na Chama cha ACT-Wazalendo huku akivitaka vyama vya upinzani kuweka ubinafsi pembeni na kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.

Aidha Membe ameiomba kambi rasmi ya upinzani nchini ambayo inaundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutambua kuwa umoja ni nguvu  hivyo wakubali kuungana ili kuiondoa Serikali iliyopo madarakani na kusisitiza kuwa milango ya Ikulu ipo wazi.

Membe ametoa kauli hiyo leo Julai 16, 2020, mara baada ya kutambulishwa rasmi kuwa ni mwanachama  wa chama hicho katika ukumbi wa Mliman City jijini Dar es Salaam.

Akizungumza ukumbini hapo, Membe amesema, vyama vyote vya upinzani vinapaswa kuacha ubinafsi, tamaa bali viungane ili viweze kuchukua uongozi wa nchi ambao upo wazi kuchukuliwa kwa mwaka huu.

“Tuache ubinafsi na tamaa bali tuungane pamoja katika ngazi ya taifa, tuende kifua mbele kuchukua uongozi wa nchi ambao barabara iko wazi nina imani na viongozi wa ACT-Wazalendo watalibeba hili,” amesema Membe huku akishangiliwa na mama ya wanachama wa Chama hicho

Membe amesema hakuna kipindi ambacho milango ya Ikulu iko wazi kama ilivyo sasa hivi hivyo amesisitiza ushirikiano ili kuhakikisha Chama hicho kinavuna wanachama wengi watakaokwenda kuwapigia kira wagombea watakaoyeuliwa na Chama hicho.

“Upinzani ukiwa na mgombea mmoja basi milango ya Ikulu iko wazi kuliko tangu tulipopata uhuru (mwaka Desemba 1961),” amesema Membe.

Hata hivyo Mwanasiasa huyo alisisitiza na kutoa  wito kwa kambi ya upinzani nchini, kuungana kwa pamoja ili kuitoa Serikali iliyoko madarakani.

“Naomba nitoe wito kwa kambi za upinzani, ni lazima tuungane ili tuweze kumtoa mtu yule Ikulu, ili tumpeleke nyumbani akapumzike na turekebishe haya mambo kama tunavyopanga kwenye mkataba wetu na wananchi,” amesema Membe.

Membe amesema, “ni vizuri kambi ya upinzani, mimi nimeingia ACT lakini kambi ya upinzani ni kubwa tukitaka tuchewele tusiende Ikulu shauri yetu, tukitaka tusiungane tusiende Ikulu shauri yetu, tuungane.”

Kilichomsukuma kujiunga na ACT- Wazalendo

Aidha Membe amesema kilichomfanya ajiunge na ACT- Wazalendo kwa sababu ni chama makini ambacho kinahitaji mabadiriko ili kusonga mbele na hatimaye kuingia madarakani.

"Kila kulipotokea jambo kubwa ACT haikukaa kimya, walipoona watu wanaonewa na kubambikiziwa kesi mahakamani hawakukaa kimya, pia walipowaona viongozi wenzao wa upinzani wanafungwa walitoka na kuzungumza wala hawakukaa kimya,

" Hongereni ACT- Wazalendo kwa kusimama kidete katika kuwatetea wanyonge na watu wote ambao hawatendewi haki," amesema

Amesema amejiunga na chama hicho pia ili aweze kufanya kazi ya uongozi na wanachama wake katika kushawishi watanzania kuleta mabadiriko nchini.

"Chama hiki ni miongoni mwa vyama vya upinzani vinavyokuwa kwa kasi kubwa hapa nchini, nimesoma katiba yao na kuona misimamo yake hasa katika suala la muungano wa Tanzania na Zanzibar," amesema

Hata hivyo Membe amesema kama wakipata nafasi ya kuingia Ikulu, watashughulikia na suala la ajira kwa vijana  na kuongeza mishahara kwa wafanyakazi.

Miongoni mwa viongozi waliompokea Membe leo Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Maalim Seif Sharrif Hamad, Kiongozi wa chama hicho Zitto Kabwe, na Katibu Mkuu wa Chama Ado Shaibu, Makamu wenyeviti wa chama hicho, Juma Duni Haji (Zanzibar) na Doroth Semu wa Bara.

Membe, alifukuzwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Februari 28, 2020 na Kamati Kuu ya chama hicho, kisha uamuzi huo kubarikiwa na Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), uliofanyika Julai 10, 2020.

Membe alifukuzwa kwa tuhuma za ukiukwaji wa maadili ya CCM, pamoja na kuonywa mara kadhaa, pasipo kubadilika.

No comments:

Post a Comment

Pages