Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi kwenye Uwanja wa Ndege wa
Nachingwea kabla ya kurejea Dodoma akitoka Ruangwa, Julai 21, 2020.
Kushoto ni Mkewe Mary Majaliwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
RAIS Dkt. John Pombe Magufuli
amewashukuru wazee wa wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi kwa mchango wao wa sh.
100,000 walioutoa ili umsaidie katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Julai 13, 2020 Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa katika uwanja wa ndege wa Nachingwea alipokea mchango huo kwa niaba ya
Rais Dkt. Magufuli kutoka kwa wazee hao.
Akitoa salamu hizo kwa niaba ya
Rais Dkt. Magufuli, leo mchana (Jumanne, Julai 21, 2020), katika uwanja wa
ndege wa Nachingwea Mkoani Lindi, Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli
amefarijika sana kwa mchango huo.
"Rais amesema aliniona
wakati napokea salamu kutoka kwa wazee hapa uwanja wa ndege Nachingwea,
mkanikabidhi mchango kwa ajili yake, anawashukuru sana na salamu zenu
amezipokea kwa mikono miwili," amesema.
Amesema Rais Dkt. Magufuli
anawashukuru kwa kupata wazo hilo na amewataka waendelee na majukumu yao na
ameahidi kuzunguka maeneo yote nchini ili kuwapa mrejesho wa utekelezaji wa
Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 - 2020.
Akizungumzia mchakato wa kura za
maoni ndani ya CCM, Mheshimiwa Majaliwa , amewapongeza wana CCM waliojitokeza
kwa wingi kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuipeperusha bendera ya CCM katika
Uchaguzi Mkuu ujao na amewataka waendelee kuwa wamoja.
“Endeleeni kuwa wamoja hata baada
ya mchakato wa kumpata mgombea mmoja wa kupeperusha bendera ya CCM kukamilika
na ninawasihihi wote muungeni mkono mgombea huyo ili kujenga mshikamano na
kukipa Chama ushindi,” amesema.
Mheshimiwa Majaliwa alisema hayo
baada ya kubaini kuwa miongoni mwa wananchi waliojitokeza kwenye Uwanja wa
Ndege wa Nachingwea kumuaga wakati akitoka Ruangwa kurejea Dodoma ni Wana CCM
waliojitokeza kuomba ridhaa ya Chama kwa nafasi ya ubunge na ambao wamemaliza
mchakato wa awali wa kupigiwa kura.
Wakati huohuo , Waziri Mkuu amewataka viongozi wa Chama na Serikali
wahakikishe wanawahamasisha wananchi kufanya kazi za kujiletea maendeleo
ikiwemo kujihusisha kwenye kilimo na biashara.
"Ndugu zangu tuendelee
kuhamasisha Watanzania na wana- Nachingwea wafanye kazi kwa bidii, lazima kila
kaya ijiridhishe inakuwa na chakula cha kutosha lakini pia ilime mazao ya
kibiashara kama korosho, ufuta, alizeti na mazao mengine, kila mmoja awe na
akiba ya kutosha ya mazao ya chakula na biashara.”
No comments:
Post a Comment