July 15, 2020

Shija R. Shija achukua fomu ya ubunge Jimbo la Mbagala

Mwanamichezo Shija Richard Shija, amechukua fomu kuwania uwakilishi wa Jimbo la Mbagala katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Shija ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Fedha ya klabu hiyo, amechukua fomu hizo katika ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Temeke, Dar es Salaam.

Alifika katika ofisi za CCM wilaya ya Temeke majira ya saa nane mchana. Hakutaka kutoa maelezo zaidi ya kusema anasubiri taratibu za chama chake zichukue mkondo wake.

"Siku kama ya leo Julai 14, 1979 mama yangu alinizaa katika ardhi ya Mbagala. Nikiwa Mwana wa Mbagala, najisikia furaha wakati ninapotimiza miaka 41 kujitoa kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wenzangu wa Mbagala. Ni kweli nimetoka kuchukua fomu. Chama chetu (CCM) kina utaratibu mzuri sana kuhusu uchaguzi wa kura za maoni. Muda ukifika nitazungumza mengi. Kwa sasa itoshe tu kuthibitisha kwamba ni kweli nimechukua fomu."

Shija ni msomi wa Shahada ya Juu ya Uhasibu (CPA), pia ana shahada ya uzamili (Masters) ya Sheria za Kodi na Utawala kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alisoma elimu ya msingi katika shule ya msingi Mbagala kuanzia 1988 hadi 1994. Mwaka 1995 alijiunga na sekondari ya Forodhani hadi 1998 alipohitimu na kujiunga na sekondari ya Mkwawa iliyopo Iringa kwa masomo ya Juu ya Sekondari mchepuo wa sayansi, PGM.

Pia alipata kusoma Stashahada ya Juu Uhasibu kutoka chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) na Stashada ya Uzamili ya Usimamizi wa Fedha kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha IFM Dar es Salaam.

Mwaka 2017 aliwania Urais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania na kushika nafasi ya pili chini ya Rais wa sasa wa Shirikisho hilo, Wallace Karia.

No comments:

Post a Comment

Pages