July 13, 2020

TALGWU YASEMA HAKUNA UBADHIRIFU KATIKA CHAMA CHAO, CHAJIPANGA KUWACHUKULIA HATUA WANAOTOA TAARIFA ZA UONGO

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU), Rashid Mtima akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).

 
Na Janeth Jovin

CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kimesema taarifa zilizosamabaa kuwa kuna ubadhirifu ndani ya Chama hicho hazina ukweli na kuongeza kuwa wanaendelea na juhudi za kutetea haki na maslahi ya wanachama wao.

Aidha TALGWU kimesema kitakichukulia hatua kali za kisheria chombo cha habari kilichochafua taswira ya chama hicho kwa kuwa taarifa hizo zilizotolewa zimeleta mkanganyiko mkubwa kwa viongozi na wanachama hadi baadhi yao kukosa imani na Chama chao.

Hayo yote yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa TALGWU, Rashid Mtima wakati akizungumza na waandishi wa habari  kuhusiana na habari wanaodai kuwa ni ya upotoshaji ambayo iliandikwa hivi karibuni na chombo kimoja cha habari hapa nchini.

Mtima amesema TALGWU  ilianzisha Taasisi ya fedha kwa lengo la kuwasaidia wanachama wake kupata mikopo kwa riba nafuu.

Amesema taasisi hiyo ya mikopo ilianzishwa na kusajiliwa kwa mujibu wa Sheria ya vyama vya wafanyakazi, hivyo  TALGWU na TALGWU Microfinance PLC,ambayo ni taasisi mbili tofauti kwa mujukumu na uongozi ni tofauti kiutendaji.

Alifafanua kwamba Oktoba 2018 uongozi wa Chama uligundua kuna changamoto kwa upande wa uendeshaji wa taasisi na uongozi uliotoa maelekezo kwa Bodi ya TALGWU Microfinance plc kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kufanyika kwa uchunguzi maalum.

"Baada ya kufanyika kwa uchuguzi huo ulipelekea watendaji wakuu wa taasisi kusimamishwa kazi na hatimaye kuachishwa kazi. Aidha bodi iliwasilisha suala hilo kwa vyombo vya dola ikiwemo TAKUKURU na Polisi na uchunguzi unaoendelea,” amesema

Akizungumzia suala la Ujenzi la Kitega Uchumi cha Chama, Mtima amesema tangu uongozi wao uingie madarakani Septemba 2016, ulikuta ujenzi huo wa kitega uchumi umesimamishwa na baada ya kushughulikia mnamo Agosti 2017, mamlaka husika ziliruhusu ujenzi huo  kuendelea baada ya kujiridhisha kwamba unakidhi viwango vya kisheria.

" Uongozi wetu haujawahi kutumia ujenzi kama kichaka cha kujipatia fedha, sisi uongozi wetu ndito umesimamia kwa karibu hatua zote za ukamilishaji wa Ujenzi na kwa sasa muda wowote mkandarasi atakabidhi jengo kwa ajili ya matumizi," amesema na kuongeza

“Tangu tulipoingia madarakani TALGWU haina madeni ya makato ya kisheria kama taarifa zinavyoeleza, bali madeni yaliyopo ni ya kawaida ya kitaasisi ambayo hayajasababishwa na ujenzi wa jengo la kitega uchumi kama taarifa zilivyodai,”amesema Mtima na kuongeza;

“Nashangaa katika taarifa hizo imesema TALGWU ilinunua samani za sh. bilioni 2, hilo si kweli bali samani zilizonunuliwa zilikuwa na thamani ya sh,. milioni 883, huku lifti ikinunuliwa kwa kiasi cha sh.milioni 980 ambayo ilijumuisha ununuzi, ufungaji pamoja na matengenezo kipindi cha matazamio,”amesema.

Amesema majukumu ya TALGWU yanatekelezwa na Chama hicho kwa mujibu wa ibara ya 1.4 ya katiba ya Chama toleo la  mwaka 2016. Kwa mujibu wa Mtima Chama hicho kipo mstari wa mbele katika utetezi wa kesi mbalimbali zinazowakabili wanachama wake kwa kutumia mawakili wa Chama, makatibu wa mikoa na mawakili wa nje.

“Akitolea mfano wa Chama kusimamia kesi za wanachama wake, amesema kimesimamia kesi takribani 130 na kesi zilizoisha zilikuwa 52.

"Chama kimefanikiwa kushinda kesi 47 huku kesi 31 zikiwa bado zinaendelea kufuatiliwa katika Mahakama mbalimbali nchini,”alisema na kuongeza;

“Mwaka 2018 Chama kilisimamia suala la watumishi waliosimamishwa kazi kwa kuwa na elimu ya darasa la saba na wote walirudishwa kazini, huku mwaka 2019 Chama kilishirikiana na TUCTA kupigania kurudishwa kwa kikokotoo cha awali na hatimaye wanachama wetu wanaostaafu wanalipwa kwa kanuni za awali."

Aidha amesema mara Kwa mara chamanhicho kimekuwa kikitoa mafunzo kwa wanachama na kutoa mfano kwa mwezi Agosti hadi Septemba 2019, yalifanyika mafunzo kwa viongozi ngazi za mikoa na matawi nchi nzima.

"Aidha kila mwezi Chama kimekuwa kikipeleka fedha za uendeshaji wa ofisi za mikoa na ruzuku za matawi," amesema

Kuhusu manunuzi ya sare za mei mosi zenye gharama za Sh. bilioni 1.1, Mtima amesema mchakato wa zabuni wa ununuaji wa sare hizo ulianza tangu Oktoba 2019 kabla ya janga la corona kutokea.

"Bodi ya zabuni  katika kikao chake kilichofanyika Januari 22 hadi 23 mwaka huu jijini Dodoma,  kiliagiza Menejimenti kukaa ma mzabuni aliyepitishwa na bodi kujadili aina ya muundo wa fulana pamoja na maboresho ya kofia na katika mabadiliko hayo iliagiza yasiathiri bajeti iliyoidhinishwa na Baraza Kuu Taifa,”amesema.

Mtima amesema baada ya menejimenti kukaa na kujadiliana na mzabuni na kuongeza ubora wa fulana na kofia,bajeti iliyotengwa na Chama haikuathirika na kiasi cha sh. milioni 147.5 kilisalia.

Amesema chama hakina ufujaji wowote wa fedha uliofanyika kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari, kwani hadi kufikia Machi 2020 chama kina wanachama 71,948.

Akizungumzia suala la vikao vya ndani, nje na vikao vya Posho,
Mtima amesema kwa mujibu wa sura ya tano ya katiba ya Chama toleo la mwaka 2016 imeainisha vikao vyote vya Chama vya kikatiba ambapo kamati ya Utendaji taifa hukutana mara nne kwa mwaka na Mkutano Mkuu wa Taifa ufanyika mara mbili ndani ya miaka mitano.

Amesema vikao vya posho vinavyoitishwa ni kwa mujibu wa Katiba ya chama na hata siku moja katibu Mkuu hajawahi kuitisa vikao visivyo rasmi au nje ya katiba, kikanuni,utaratibu na bajeti ya Chama.

Mtima amesema tangu uongozi wao uliopo madarakani uingie kazini Septemba 2016, Ofisi ya Katibu Mkuu imekuwa ikitimiza takwa la kikatiba na kuitisha vikao hivyo kwa miaka mitatu mfululizo.

Hata hivyo amesema TALGWU linawataka waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa kuzingatia taaluma na maadili ya uandishi ili kuhakikisha kuwa wanapata habari kutoka pande zote kabla ya kuandika au kuripoti taarifa.
 

No comments:

Post a Comment

Pages