July 24, 2020

TASAC kuadhimisha siku ya bahari Afrika, yasema Serikali itaendelea kupambana na uvuvi haramu

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Emmanuel Ndomba, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.


Na Janeth Jovin


SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limesema kuwa katika kuadhimisha siku ya bahari Afrika, Serikali itaendelea na malengo ya  kupambana na uvuvi haramu unaotumia baruti na sumu baharini, utupaji wa taka za plastiki, biashara ya mafuta ya magendo inayofanyika majini, uharamia pamoja na ujambazi wa silaha dhidi ya meli.

Aidha Shirika hilo limesema Serikali itaendelea pia kupambana na umwagaji wa mafuta baharini, biashara ya silaha, dawa za kulevya, magendo na kuongeza kuwa watazingatia malengo hayo kama yalivyoainishwa na Kamisheni ya Umoja wa Afrika (CAU) kwenye maeneo ya bahari na maziwa.

Hayo yote yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Emmanuel Ndomba wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya maadhimisho ya siku hiyo itakayoadhimishwa kesho kwa wafanyakazi wa Shirika hilo kwa kushirikiana na wadau wengine kufanya shughuli mbalimbali za kijamii zisizokuwa na mikusanyiko kwa lengo la kuchukua tahadhari ya virusi vya Corona.

Ndomba amesema Serikali itazingatia pia katika ufanyaji wa utafiti, ubunifu, uendelezaji wa uchumi endelevu wa bahari, utafutaji wa mafuta na gesi baharini, tabia nchi, ulinzi wa mazingira, uhifadhi pamoja na uchukuzi salama baharini.

"Malengo ya maadhimisho haya yana nia njema na muhimu kwa taifa katika kuliongezea uwezo na ufanisi wa kutumia rasilimali zinazopatikana kwenye bahari, maziwa na mito ili kukuza uchumi wa nchi.

"Nitoe wito wa kuendelea kushirikiana kikamlifu kwa kutekeleza maazimio haya, mikataba ya kimataifa itakayorodhiwa na Serikali yetu ya Tanzania, " amesema Ndomba.

Amesema Tanzania ni nchi yenye ukanda mkubwa bahari ya Hindi wenye urefu wa Kilomita 1426 kutoka mkoa wa Tanga mpaka mkoani Mtwara, pia inazungukwa na maziwa makubwa kama ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa.

"Mazingira haya yanavutia kuyatumia vema kwa kuwa na sera, sheria na utekelezaji mzuri ambao utapelekea kuwa nchi yenye ulinzi, usalama na uchumi wa bahari ili kuendelea kuvutia na kuinua biashara ya meli ambayo ni endelevu," amesema

Kuhusu maadhimisho ya siku ya bahari Afrika, Ndomba amesema yataendelea kuwa chachu ya kuibua fursa kwa wadau, wananchi na wataalamu mbalimbali wanaofanya kazi kwenye sekta ya bahari.

"Tumeshapata matokeo chanya baada ya Serikali ya Tanzania bara na Zanzibar kuendelea kuwekeza katika miradi mikubwa nchini ikiwemo miradi inayoendelea kutekekezwa ambayo ni upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, ghati ya Kabwe na Kasanga katika ziwa Tanganyika.

"Pia ujenzi wa Chelezo ya Meli Mwanza South, ziwa Victoria, ujenzi wa meli kubwabya abiria na mizigo na ukarabati mkubwa wa Meli ya MV. Victoria na Mv. Butiama, ununuaji wa meli ya mizigo na abiria MV. Mapinduzi II na MT. Mkombozi II ambayo ni ya kubebea mafuta na gesi, hivyo kuna fursa nyingi za kiuchumi zimeletwa na miradi hii iliyopo na ijayo," amesema

Amesema maadhimisho ya mwaka huu yataadhimishwa kwa kauli.mbiu inayosema 'ubunifu katika matumizi endelevu ya bahari'.

"TASAC, Mamalaka ya Bahari Zanzibar na wadau wote tunaadhimisha siku hii kwa kutumia njia ya Tehama na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii zisizokuwa na mikusanyiko ya watu wengi kwa lengo la kuchukuwa tahadhari ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID-19)," amesema

Naye Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Dk. Erick Masami amesema anatoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri majini kujitokeza kwa wingi kusoma katika chuo hicho ilikupata ujuzi wa kutosha wa namna ya kukutumia vyombo hivyo.

No comments:

Post a Comment

Pages