July 26, 2020

THRDC: Uhuru wa kujieleza ndio msingi wa haki zote nchini

Na Janeth Jovin


Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umesema kuwa wadau mbalimbali wanapaswa kushirikiana katika kuhakikisha haki za msingi na sheria kandamizi zinafanyiwa marekebisho ili uhuru wa kujieleza uendelee kuwepo sehemu kubwa ya Tanzania.

Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam na Mratibu wa Kitaifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa wakati akifunga mafunzo ya siku tatu yaliyokutanisha waandishi wa habari, wanasheria na wadau mbalimbali wa haki za binadamu.

Olengurumwa amesema uhuru wa kujieleza ndio msingi wa haki zingine zote hapa nchini hivyo ni muhimu wadau hao kushirikiana kutokemeza sheria zote kandamizi zinazozuia kuwepo kwa uhuru huo.

Amesema uhuru wa kujieleza aupaswi kuwepo kwa wanasheria,  wanaharakati na waandishi wa habari tu bali ni kwa ajili ya watanzania wote.

“Ninyi waandishi wa habari na wanaharakati  mmekuwa mkitafuta habari ili kuweza kuzitoa hivyo mara nyingi uhuru wa kujieleza unaonekana kama ni wa kwenu peke yenu kuupata, lakini kimsingi uhuru wa kujieleza ni haki ya kila mtu.

“Mfano mtoto akifanyiwa ukatili ana haki ya kueleza kilichotokea na huo ndio uhuru wa kujieleza, mtu akifanyiwa kitua ambacho si kizuri na kutaka kuongea huo ndio uhuru tunaosema,” amesema

Olengurumwa amesema ili mtu aweze kutetea haki za watu wengine ni muhimu kuwepo kwa uhuru wa kujieleza na kuongeza kuwa sehemu yeyote ambayo haina jambo hilo ni rahisi haki za jamii mbalimbali kuminywa.

Amesema anaamini kuwa wale waliofanikiwa kushiriki katika mafunzo haya watakwenda kuibadirisha jamii huku wanasheria kuwa na uwezo kwa kusimamia na kutetea na hatimaye kushinda kesi zote za waandishi na uhuru wa vyombo vya habari.

 Naye Mjumbe wa bodi ya THRDC, Keneth Sembaya amesema mafunzo hayo yaliyotolewa ni muhimu kwa wanasheria hasa katika kuwajengea uwezo wa kusimamia kesi zao za kutetea haki za binadamu.

“Mabadiliko hayawezi kutokea kama tutatazama mabo kama yalivyo bali tumieni mafunzo haya vizuri hasa katika kuhakikisha mnaisaidia jamii kwenye utetezi wa kesi mbalimbali zinazowakabili,” amesema

No comments:

Post a Comment

Pages