July 28, 2020

UWANJA WA MICHEZO TAIFA WABADILISHWA JINA SASA BENJAMIN WILLIAM MKAPA STADIUM



Na Shamimu Nyaki – WHUSM
Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli ametangaza rasmi kuwa kuanzia leo Julai 29, 2020 Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam utaitwa Uwanja wa Uwanja wa Benjamin Mkapa (Benjamin Mkapa Stadium) ili kuendelea kumuenzi Rais huyo wa awamu ya Tatu.

Rais Magufuli ametoa tamko hilo katika hafla ya kuaga mwili wa aliyekuwa rais wa serikali ya awamu ya tatu Hayati Benjamin William Mkapa iliyofanyika katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam ambapo alisisitiza Mzee Mkapa alikuwa na mchango mkubwa katika sekta ya michezo nchini hivyo taifa tunapaswa kumuenzi.

“Mzee Mkapa aliujenga uwanja mkubwa wa michezo na alikua hapendi vitu viitwe kwa jina lake, lakini kwakuwa kwa sasa amelala na hawezi kuniadhibu na kwakua nimepokea meseji nyingi nimekubali na sasa natamka rasmi uwanja ule uitwe Mkapa Stadium,”Dkt.Magufuli.

Dkt.Magufuli ameongeza katika Michezo Mzee Mkapa alikuwa  anapenda sana michezo ndio maana amefanya mambo mengi sana katika sekta hiyo,vile vile alikua ni Shabiki wa Timu ya Yanga japo hakuwahi kuonyesha hadharani hivyo tunapaswa kumkumbuka na kutunza kumbukumbu   hizo.

Hata hivyo Uwanja wa Taifa Dar es Salaam (Mkapa Stadium) ni miongoni mwa viwanja vikubwa barani Afrika ambavyo vimekidhi vigezo vyote vilivyoanishwa na Shirikisho la Soka Duniani FIFA na una uwezo wa kuingiza mmashabiki takriban elfu sitini.

Hivi karibuni watu wengi walionyesha nia yao ya kuomba uwanja huo uitwe jina la Mzee Mkapa kama njia ya kumuenzi Rais huyo mstaafu ambayo leo Mhe.Rais ameitimiza nia hiyo.

Pamoja Mheshimiwa Rais Magufuli aliendelea kusisitiza kuwa Mzee Mkapa katika sekta ya Sanaa napo ameacha alama kwani ndiye aliyeanzisha Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki (COSOTA) ambayo kwa sasa ni taasisi rasmi lengo ni kuwasaidia wasanii kupata haki za kazi zao na katika sekta ya Habari ndiye muasisi wa Vitengo vya Habari na Mawasiliano katika wizara.
Naye mmoja wa wananchi na shabiki wa mpira nchini Bw.Athuman Ugassa amepongeza uamuzi Mheshimiwa Rais Magufuli wa kuupa uwanja huo jina lake kwani uwanja huo ni alama ya mchango wake katika kuendeleza sekta ya michezo nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages