July 24, 2020

WADAU WATAKIWA KUTUNZA VYANZO VYA MAJI


Mwenyekiti Bodi ya Maji ya Taifa Professa Hudson Hamisi Nkotagu amewataka wadau wa sekta ya maji nchini kuhakikisha wanatoa elimu ya utunzaji wa vyanzo vya maji ili kuwawezesha wananchi kutambua na kushiriki kikamiifu katika zoezi hilo. Amesema wananchi wamezungukwa na fursa nyingi ambazo wanaweza kuzitumia iwapo tu watawezeshwa kuzitambua.

Wito huo ameutoa leo wakati wa ziara ya Bodi ya maji ya Taifa kukagua hatua mbalimbali zinazofanywa na wadau wa sekta ya maji katika kulinda na kuendeleza vyanzo vya maji nchini ziara ambayo imefanyika mkoani Tanga.


Amesema wananchi ni wadau muhimu katika kufanikisha zoezi la utunzaji na uendelezaji wa vyanzo vya maji iwapo tu wataelimishwa na kupewa njia mbadala itakayowawezesha kujikimu kimaisha badala ya kuwabana kwa kutumia sheria peke yake.


“Kama tunataka kutunza mazingira yetu ili yawe endelevu isiwe tu kutumia sheria kuwabana wananchi bali waelimishwe na kupewa njia mbadala ya kujiongezea kipato ambayo vilevile inaweza kuwa inasadia kutunza mazingira.”


Awali akikagua Bwawa la ufugaji wa samaki katika Kijiji cha pande Halmashauri ya Jiji la Tanga Afisa Maendeleo ya Jamii Jiji la Tanga Bi. Zuwena Kilavu amesema Jiji hilo limewezesha kupunguza kwa kiasi kikubwa uharibifu wa maji katika Mto zigi ambao ni tegemeo kubwa kwa wananchi baada ya kuwaelimisha wananchi  na kuwajengea Bwala Kijiji hapo.


“Wananchi walikuwa wakichimba mchanga katika mto Zigi hali ambayo ilikuwa ikisababisha uharibifu mkubwa wa mazingira, baada ya kuwajengea Bwawa hili uharibifu umepungua sana na unaelekea kuisha kabisa. Amesema Zuwena.

Kwa upande wao wananchi wa Pande wameishukuru serikali kwa kuwajali na kwamba walikuwa wakipambana na hatari nyingi wakati wa kutafuta mchanga mtoni. 

Mwenyekiti wa Kikundi hicho chenye jumla ya wanachama 45 amesema kuna baadhi ya wenzao walipoteza Maisha kwa kuliwa na mamba wakati wa shughuli ya kutafuta mchanga mtoni, huku Mkurugenzi wa Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvu, Emmanuel Bulai akisema miradi ya Mabwawa ni njia nzuri ya kuondoa uharibifu wa mazingira na amewataka wananchi kufuata miongozo ya ujenzi wa mabwawa hayo ili kuepuka uharibifu Zaidi wa mazingira.

No comments:

Post a Comment

Pages