July 31, 2020

Wavunaji misitu kinyume cha sheria ni majingili-TAKUKURU

Na Goodluck Hongo

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rishwa (TAKUKURU) imesema watu wote watakaokamatwa kwa kosa la kukutwa na  rasilimali za misitu watashitakiwa  kama majangili wa wanyamapori wahujumu uchumi.

Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam na Afisa Mwandamizi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Ally Katonya wakati akitoa mada katika mjadala wa masuala ya ujangili wa wanyamapori uliondaliwa na Chama cha Waandishi wa habari za Mazingira (JET)  kwa kushirikiana na USAID Protect.

Anasema rasilimali za misitu ni nguvu kubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa lakini kumekuwa na uvamizi mkubwa wa rasilimali hizo kupitia kilimo,uchomaji wa mkaa,uchimbaji wa madini katika maeneo ya misitu.

“Waandishi wa habari wamekijikita sana katika ujangili wa wanyamapori lakini kukatwa kwa misiti nako pia ni ujangili kwani kunaadhiri wanyamapori hivyo sisi kama TAKUKURU tunasema yeyote anayeshitakiwa kwa mazao ya misitu ni jangili kama walivyo majangili wa wanyamapori”anasema Katonya

Anasema Tanga ndio Mkoa unaoongoza kwa kupitisha mazao ya misitu ikiwemo baadhi ya miti ambayo inahitajika sana nchini China wa Mkunungu ambapo badhi ya mikoa kama Katavi na Tabora ndio inayoongoza kwa uvunaji wa mazao ya misitu.

“Misitu ni kitu muhimu sana kwenye uhifadhi wa wanyamapori na ni sekta ambayo inaingiza fedha nyingi lakini kukatwa kwa miti hiyo, ni wanyama wangapi wamekimbia au kuhama kutoka maeneo hayo muhimu,  hivyo hiyo nayo ni ujangali”anasema Katonya

Katonya anaongeza kuwa hata wasimamizi wa sheria wakidanganya kwa kutoeleza ukweli juu ya vibali vilivyotolewa vya uvunaji wa misitu nao watashitakiwa kama majangili wa uhujumu uchumi.

“Tunawaomba waandishi wa habari kusaidia katika eneo hili la misitu kwani asilimia 60 ya Ikolojia ya Tanzania iko katika Kanda ya Magharibi inayonundwa na baadhi ya mikoa kama  Tabora na Katavi ambapo pia ndio maeneo ambayo misitu inavunwa kwa wingi” anasema Katonya

Kwa upande wake mwakili kutoka Taasisi ya  Sekta Binafsi (TPSF)  Victoria Michael anasema Sekta Binafsi iliachwa nyuma katika masuala ya uhifadhi wa mazingira.

Anasema majangili wamekuwa wakitumia fedha hizo haramu kuingiza katika mzunguko kupitia benki hivyo ikiwa Sekta Binafsi itabaki nyuma mapambano hayo hayawezi kufanikiwa.

Akizungumzia kuhusu hilo,Mwenyekiti wa JET Dk.Hellen Otaru anasema lengo la mjadala huo ni kuhakikisha waandishi wa habari wanajifunza na kuwa na uelewa mkubwa juu ya ujangili wa wanyamapori na mazingira yao.

“Sisi kama wanahabari ni wajibu wetu kusaidia jamii katika kutoa taarifa sahihi juu ya masuala ya ujangili wa wanyamapori na mazingira yao kwa kufikisha elimu hiyo kwa watanzania ili kuhakikisha kuwa ujangili dhidi ya wanyamapori unaisha”anasema Dk.Otaru

Mkurugenzi Mtendaji wa JET John Chikomo anasema chama hicho kitaendelea kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari katika suala zima la utunzaji wa mazingira,utalii na ujangili wa wanyamapori kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

No comments:

Post a Comment

Pages