July 16, 2020

Wizara yatoa mafunzo kwa wachuna ngozi zaidi ya 700

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Katika jitihada za kuhakikisha kuwa thamani ya ngozi inaongezeka, Wizara ya Mifugo na Uvuvi mpaka sasa imetoa mafunzo kwa wachunaji wa ngozi za wanyama takriban 735 nchini.


Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo, Usalama wa Chakula na Lishe, Gabriel Bura katika kikao cha Wadau wa Mfuko wa Maendeleo ya Mifugo (LDF) cha kutathimini athari za ugonjwa wa Korona katika tasnia ya ngozi kilichofanyika jijini Dodoma Julai 14, 2020.


Akitoa ufafanuzi kuhusu hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara katika kuongeza thamani ya zao hilo la ngozi, Bura alisema kuwa mafunzo hayo ya wachunaji ngozi yametolewa katika Mikoa ya Kilimanjaro, Manyara, Arusha, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Morogoro na Kagera, huku akiongeza kuwa tayari mchakato wa kutoa leseni kwenye mikoa hiyo umeshaanza.


“Pia tumeanza kugawa visu vinavyotakiwa kitaalam kwa ajili ya kazi ya uchunaji katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara na mchakato wa kuhakikisha vinafika katika kanda zote tulizotoa mafunzo unaendelea,”alisema Bura.


Aliongeza kuwa hatua inayosubiriwa hivi sasa ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi kusaini nyaraka za uteuzi wa wakaguzi wa ngozi waliopatikana kutoka kwenye Halmashauri 113 ambao tayari wameshapitishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mara baada ya taratibu kukamilika wataalam hao watakuwa na jukumu la kuhakikisha wanasimamia ubora wa ngozi kama walivyoainishwa kwenye sheria namba 18 ya masuala ya Ngozi.
 

Awali, akiongea wakati wa kufungua kikao hicho, Mkurugenzi wa Masoko na Uzalishaji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Felix Nandonde alibainisha kuwa kufuatia ugonjwa wa Korona, hivi sasa ngozi inayozalishwa hapa nchini haiendi nje ya nchi na hata kama inaenda sio kwa kiwango kile cha mwanzo.

“katika kikao hiki mbali na kujadili matumizi ya fedha pia kitumike kujadili mbinu za kuikwamua tasnia hii ya ngozi kutoka kwenye hali iliyopo kwa sababu mpaka sasa nchi yetu inaagiza zaidi ya pea milioni 52 za viatu huku uwezo wetu wa kuzalisha viatu ukiwa ni milioni 1.2 tu kwa mwaka,” Alisisitiza Dkt. Nandonde.


Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar-es-salaam (DIT) Tawi la Mwanza, Dkt. Albert Mmari alisema kuwa taasisi yake ilishaanza kuchukua hatua kadhaa za kuongeza thamani kwenye tasnia ya ngozi ikiwemo kuongeza mashine za mafunzo ya kutengenezea viatu ambapo mpaka sasa zipo 50 ukilinganisha na 25 zilizokuwepo hapo awali.


“Kupitia kikao hiki ninapenda kuwataarifu kuwa taasisi yetu kupitia benki ya dunia imepata zaidi ya shilingi bilioni 37 ambazo zitatumika kwenye mradi wa miaka 5 ya kuboresha miundombinu ya chuo ikiwemo kununua mashine za kisasa za kufundishia, studio za kubuni mitindo mipya ya viatu na bidhaa nyingine zitokanazo na ngozi, kujenga madarasa ambapo mara baada ya kukamilika kwa madarasa hayo yatakuwa na uwezo wa kubeba wanafunzi zaidi ya
1000” Alifafanua Dkt. Mmari.

Wadau waliohudhuria kikao hicho walitoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda na Biashara, Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Taasisi ya Teknolojia Dar-es-salaam(DIT) tawi la Mwanza.

No comments:

Post a Comment

Pages