August 19, 2020

Ruth Zaipuna - Afisa Mtendaji Mkuu Mpya wa Benki ya NMB

Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya NMB imemtangaza, Ruth Zaipuna, kuwa Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Benki hiyo uteuzi ulioanza jana Agost 18,2020. Mwenyekiti wa Bodi ya NMB – Dk. Edwin Mhede alimtangaza Zaipuna huku akikiri kuwa mchakato wa kumpata haukuwa mwepesi lakini hakukuwa na upendeleo isipokuwa walitazama wasifu, utendaji na maslahi ya Benki na Tanzania.


Dk. Mhede alisema katika kipindi kirefu Benki hiyo ilikosa mtu baada ya aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wake kuondoka na hivyo walibaki na mtu aliyekuwa anakaimu kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu lakini takwa la kisheria lilikuwa linawabana kuwa ni lazima wapate mtu.
 

Zaipuna anakuwa Mtanzania wa kwanza kushika nafasi hiyo tangu Benki hiyo ilipobinafsishwa ambapo kwa nyakati zote nafasi za juu zilishikwa na wageni wakiwemo Ineke Bussemaker aliyekuwa Mkurugenzi tangu 2014 – 2018 kisha nafasi hiyo ikachukuliwa na Albert Jonkergow ambaye alishikiria kwa kipindi cha mpito cha miezi sita kabla ya Zaipuna kupewa nafasi ya kukaimu.


Mwenyekiti alisema mchakato wa kumpata Mtendaji Mkuu ulikamilika Juni 30,2020 na jana ilikuwa ni siku ya kumtangaza huku akibainisha kuwa sifa zote zilizotakiwa katika nafasi hiyo, walijiridhisha kuwa Zaipuna anazo hivyo hakuna shaka kuhusu utumishi wake katika nafasi hiyo.


‘’Katika kipindi chote tulihangaika kumpata mtu mwenye kufikia vigezo vinavyotakiwa, lakini wakati mwanamama huyu alipokuwa anakaimu, Benki imeendelea kufanya vizuri zaidi na kukuza mtaji wake, hakuna mahali paliyumba chini ya usimamizi wake,hivi kwa hali hiyo mnadhani tungefanyaje,’’alisema Dk. Mhede.
 

Alitaja mafanikio makubwa katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu wa kukaimu kwa Afisa huyo ni faida kubwa ambayo benki imekuwa ikipata ikiwemo Sh.93 bilioni zilizopatikana katika kipindi cha nusu ya kwanza ya 2020 huku mahusiano yakizidi kuimarika kati ya benki na Serikali pamoja na wateja wake. 

 

Hata hivyo alimuagiza mtendaji huyo kuhakikisha benki inaendelea kuwa imara na yenye kutoa matumaini kwa wananchi wake huku akisisitiza ushirikiano wa timu moja kati ya kiongozi huyo na watumishi wengine ndani ya taasisi yao.


Akizungumza mara baada ya kupokea uteuzi huyo, Zaipuna alisema ni uteuzi wa ushindi kwa NMB wala siyo yeye lakini akaahidi kwamba atakuwa mtumishi kama ilivyo kwa watumishi wengine kwani anaamini kila mmoja anamchango wake kwa nafasi yake hivyo akaomba wenzake kujitoa zaidi katika kuwahudumia Watanzania.


Zaipuna alitaja vipaumbele vitano atakavyo anza navyo ikiwemo NMB kuendelea kukua kila mwaka na kuwa Benki namba moja nchini,Benki kuendelea kuwa chaguo la wateja, kuongeza na kuimarisha mashirikiano kwa wateja na watumishi na kipaumbele cha tano ni kuendelea kuboresha maslahi kwa watumishi ili vijana wa Kitanzania wavutiwe na kutamani zaidi waajiriwe NMB.


Alisema hayo yote yatawezekana ikiwa kila mtumishi atakuwa na nidhamu ya utekelezaji na kujituma katika ubunifu wa ushirikishwaji wa mipango lakini kwa upande wake akasema ataendeleza kasi iliyopo ili misingi iliyojengwa isiyumbe.


Kuhusu wanahisa aliitaja Serikali ya Tanzania na wabia wa benki ya Rabo ya Uholanzi kwamba waondoe hofu kuhusu NMB kwani ni chombo kilichosimama kwa ajili ya kutoa matumaini kwa watu hivyo wataendeleza kasi hiyo wakati wote.


Awali Mjumbe wa Bodi Margaret Ikongo aliwataka wajumbe kutoa ushirikiano mkubwa kwa CE0 wao mpya kwa kuwa kazi anayokwenda kuifanya ni kubwa na ndiye mbeba maono wa chombo hicho hivyo ushindi wake utategemea nguvu ya pamoja na watumishi ikiwemo kumuombea.

Bi.Ikongo alimtaka Zaipuna kufanya kazi kwa kuwashirikisha zaidi watumishi wenzake na atambue kuwa kila mmoja ana mchango mkubwa kwa sehemu yake lakini akaomba watumishi kumuombea kiongozi huyo katika cheo hicho kipya alichokabidhiwa.

No comments:

Post a Comment

Pages