August 12, 2020

SERIKALI ZA VIJIJI ZIACHE WAZI SHOROBA ILI KUONDOA MIGOGORO

 Na Goodluck Hongo

SERIKALI  za Vijiji nchini zimetakiwa kuacha wazi njia  za wanyamapori (Shoroba) wanazotumia kuhama kutoka eneo moja hadi lingine ili kupunguza migogoro baina ya wananchi  na viumbe hao. 

 

Ombi hilo limetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi  Bora  ya Ardhi Dk.Stephen Nindi wakati akitoa mada katika mkutano uliowakutanisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini juu ya uhifadhi wa mazingira na  kuondoa ujangili wa wanyamapori. 

 

Mkutano huo ambao ulifanyika kwa njia ya mtandao uliandaliwa na Chama  cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET) kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Marekani katika mradi wake wa USAID PROTECT. 

 

Anasema kati ya mambo muhimu ambayo ofisi yake inashughulika ni pamoja na kuhakikisha kuwa ardhi yote ya Tanzania inatumika katika uwiano wa usawa kwa kuwa kukiwa na matumizi ya upande mmoja huleta migogoro mingi.

 

Anasema  kwa sasa Shoroba nyingi (mapito ya wanyamapori) zimekuwa zikipitia changamoto nyingi ambapo wakati mwingine serikali za vijiji zimekuwa zikiapa kulinda maeneo hayo. 

 

Anasema  kwa sasa wanafanyakazi katika mpango maalum kwa kushirikiana na Hifadhi za Taifa (TANAPA) juu ya mpango wa matumizi bora ya ardhi katika Vijiji vyote vinavyozunguka hifadhi hizo nchini ili kuondoa migogoro ya ardhi.

 

“Serikali za Vijiji ziache maeneo ya mapito kwa wanyamapori ili wanyamapori hao waweze kupita kutoka eneo moja hadi lingine kwa kuwa wanyamapori wana mifumo yao ya kuishi lakini pia wanaweza kuishi karibu na binadamu ikiwa njia zao wanazotumia kuhama hazitafungwa”anasema Dk. Nindi.

 

Anasema kwa sasa wanashughulikia kufungua shoroba ya Udzungwa kuelekea Pori la Akiba la Selou kwa kushirikina na Taasisi ya STEPH na Serikali ya Mkoa wa Iringa ili kuafanya wanyamapori kupita katika njia zao za asili. 

 

Dk.Nindi anafafanua kuwa wanyamapori hasa Tembo hukumbuka kizazi cha babu zao hivyo hurudi katika maeneo waliyokuwa wakipita ama kuishi ambayo kwa sasa tayari kuna makazi ya binadamu.

 

“Wanyama wengi walikuwa hawaonekani sababu walikuwa wanajificha kwa kuhifia kuuawa lakini serikali ya awamu ya tano imewahakikishia ulinzi na ndio maana wanajitokeza tofauti na miaka ya nyuma ambapo Tembo walifikia 45,000 tu kutoka 350000  miaka ya Uhuru”anasema Dk. Nindi.

 

Dk.Nindi anafafanua kuwa Ofisi yao inafanya kazi na Taasisi mbalimbali za serikali na kufuata sheria ili kuhakikisha kuwa  migogoro ya ardhi inaondoka na kuwa na matumizi bora ya rasilimali hiyo.

 

Kwa upande wake Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) Dk.Iddi Lipende anasema asilimia 60 ya magonjwa yanayotokea yana asili ya wanyama. 

 

“Ni lazima wananchi waelimishwe kukaa mbali na wanyama kwani kuna magonjwa ambayo yakiambukizwa kwa binadamu ni ngumu kuyaondoa kama ilivyo Ebola  na wengi hawajui kuwa wanyama nao wanamagonjwa kwa kuwa hata nyama wanayokula haipwi hivyo kusababisha magonjwa kwa binadamu ”anasema Dk. Lipende.

 

Mkurugenzi Mtendaji wa JET John Chikomo anasema chama hicho kitaendelea kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari katika suala zima la utunzaji wa mazingira,utalii na ujangili wa wanyamapori kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

No comments:

Post a Comment

Pages