August 13, 2020

THRDC, TLS yawanoa mawakili 30 kukabili kesi za kikatiba, uchaguzi 2020

Mawakili 30 wakiwa katika picha ya pamoja na majaji wastaafu pamoja na viongozi kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika TLS na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu mara baada ya kumalizika kwa mafunzo.


Na Janeth Jovin

MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binaadam (THRDC) umesema bado nchi ina uhitaji wa mawakili wengi watakaoweza kushughulikia na kuendesha kesi za kikatiba na mashauri ya malalamiko ya Uchaguzi.

THRDC umesema ili jambo hilo lifanikiwe wao pamoja na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kimewaongezea ujuzi mawakili juu ya kuweza kushughulikia kesi hizo na zingine zinazohusiana na uchaguzi.

Mafunzo hayo yalianza kutolewa juzi Agoati 11 na Kumalizika jana Agosti 12, 20202 jijini Dar es Salaam ambapo jumla ya mawakili na  wanasheria wapatao 30 kutoka maeneo mbalimbali nchini wamepatiwa mafunzo hayo.

Mafunzo hayo yameendesha na Jaji Mstaafu Profesa John Ruhangisa na Jaji Mstaafu Robart Makaramba.

Akizungumza wakati wa THRDC, Onesmo Olengurumwa amesema kwa sasa nchi ina mawakili wachache wanaoweza kushughulikia kesi za kikatiba na uchaguzi hivyo waliona ipo haya ya kuweka mafunzo hayo  ili wataalamu hao waweze kupata uwezo wa kuzikabili vema kesi hizo hasa wakati wa uchaguzi mkuu itakapomalizika.

"Tunahitaji kupata mawakili wengi watakaoweza kuendesha kesi za kikatiba na uchaguzi, tunajua kuwa mara baada ya Uchaguzi mkuu kumalizika kesi za malalamiko kuhusu uchaguzi zitakuwa nyingi hivyo ni vema wataalamu wengi wakapa uelewa wa namna ya kuzisimamia ili waweze kuwasaidia vema wananchi.

Aidha amesema kuwa ili kesi hizo ziende haraka ni muhimu kuwepo kwa mawakili wenye uweledi sambamba na majaji na mahakimu waadilifu.

Naye  Rais wa TLS Dk. Rugemeleza Nshala amesema kuwa wanasheria wanatakiwa kupatiwa mafunzo mara kwa mara kutokana na mabadiliko ya sheria na ya kiutawala.

Amesema mwaka huu ni  wa uchaguzi hivyo kutakuwa na kesi nyingi za malalamiko ya uchaguzi hivyo mawakili wasiishie kufungua kesi na kuondolewa mahakamani katika hatua za awali badala yake zifike hadi mwisho.

" Mawakili waliopata mafunzo haya watayatendea haki kwani kwa walio wengi wao wamepata bahati ya kufunza na magwiji wa taaluma hii ya sheria"amesema Dk. Nshala.

Amesema kuwa nchi inaendeshwa kidemokrasia wananchi wote wanatakiwa kuwa chini ya sheria vilevile mahakama itoe haki na kuongeza  kuwa mfumo huo ukiimarika imani kwa wananchi juu ya chombo hicho cha utoaji haki inaongezeka.

Aidha Dk. Nshala ametoa rai kwa mawakili kuitazama fursa nyingine ya kisheria ambayo ni kifungua kesi kwenye mahakama ya Afrika Mashariki au Mahakama ya Afrika huku akiwaeleza kuwa ili waweze kuendesha kesi katika mahakama hizo za nje wanapaswa kuwa na weledi.

Kwa upande wake Profesa Ruhangisa aliyekuwa mkufunzi katika mafunzo hayo, amesema kuwa anauzoefu wa muda mrefu kwenye sheria hasa kutokana na ushiriki wake katika kuziandika na kutumikia ujaji wa mahakama kuu na ule wa  mahakama ya Afrika Mashariki.

Amesema kuwa amewafunza wanasheria mbinu mbalimbali za kisheria hasa kwenye mashauri ya malalamiko ya uchaguzi na kwamba wakishindwa kwenye mahakama za ndani waende kwenye mahakama za nje ikiwemo ile ya Afrika Mashariki au ile ya Afrika.

Naye Jaji Makaramba amesema kuwa amewaelekeza wanasheria hao namna ya kuendesha mashauri ya kiuchaguzi ambayo ni maslahi ya umma na kwamba kuna matarajio wa kuwepo kwa kesi nyingi za kiuchaguzi mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Pages