August 01, 2020

URATIBU WA KARIBU HUDUMA NDOGO ZA FEDHA KUCHANGIA KUDHIBITI MATAPELI

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Tutuba (kulia) akipata maelezo ya Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha kutoka kwa Mtaalamu wa Huduma hizo wa Wizara ya Fedha na Mipango, Joseph Msumule (wa pili kushoto), alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango, katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa, Viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.



Na Peter Haule, WFM, Simiyu


Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Tutuba, ameishauri Wizara ya Fedha na Mipango na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuratibu kwa karibu vikundi vinavyotoa huduma ndogo za fedha vikiwemo VIKOBA ili kutoa elimu na ufahamu kabla ya mwananchi kujiunga au kukopeshwa fedha ili kuwa na uhakika na usalama wa fedha.

Rai hiyo imetolewa na Bw. Tutuba, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha na Mipango wakati wa Ufunguzi wa Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nyakabindi, Mkoani Simiyu.

“Kuna vikundi vinavyowaambia wananchi kuwa vinatoza riba ya asilimia tano, kumbe asilimia hiyo ni kwa mwezi na sio kwa mwaka ukifanya hesabu utagundua  riba kwa mwaka ni asilimia 60  ilihali kuna benki zinazotoa mikopo kwa riba ya asilimia 18 kwa mwaka, hivyo lengo la huduma ndogo za fedha kumsaidia mwananchi kurahisisha shughuli za kiuchumi halifikiwi”, alieleza Tutuba.

Tutuba alisema kuwa, kuna vikundi wananchi wanaunganishwa bila kuwa na ufahamu wa kutosha hivyo kuchangishwa fedha lakini akienda kudai maslahi yake anaambiwa fedha hazipo, jambo ambalo taasisi zinazodhibiti vikundi hivyo zinabidi kufuatilia kwa karibu kwa kutoa elimu toshelevu ili mwananchi aweze kufanya maamuzi sahihi.

Pia alisema kuwa kwa ngazi ya Halmashauri anashauri fedha zinazotolewa kama mikopo kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na Wlemavu, zitolewe kwa mfumo wa kibenki utakaosaidia ufuatiliaji na urejeshwaji wa mikopo hiyo kwa urahisi kwa kuwa na uelewa wa maana ya mikopo.

Alisema kuwa kuna vikundi ambavyo vinaanzishwa kwa mtazamo wa kutafuta fedha bila kuwa na wazo au biashara yenye tija kwa kikundi na eneo alipo hivyo dhana ya kuwakomboa wananchi kupitia mikopo hiyo kutofikiwa.

“Wale wanaokopeshwa wakipata fedha katika mifumo ya kibenki watapata elimu inayotakiwa, watarejesha fedha kwa uhakika, watafuatiliwa lakini hata dhamana sio lazima ziwe za ajabu zaidi ya muhtasari wa Kijiji kutambua biashara yake”, aliongeza Tutuba.

Alisema ikiwezekana ianzishwe Benki katika Serikali za Mitaa itakayosaidia kutoa fursa kwa watu kutoa wazo la mradia au biashara na litakapodhibitishwa lina tija katika uchumi wa Kijiji au Kata linaweza kudhaminiwa na Serikali ya Kijiji ili watu waweze kurejesha fedha.

Alifafanua kuwa Benki hiyo itawahudumia wananchi kwenye maeneo yao badala ya kuwaacha wananchi kwenda kurubuniwa kwenye vikundi vyenye dhamira ovu.

Kwa upande wake Mtaalamu wa Masuala ya Sekta Ndogo ya Fedha wa Wizara ya Fedha na Mipango, Joseph Msumule, alisema kuwa Sheria mpya ya huduma ndogo za fedha imeanzishwa ili kurahisisha utoaji wa huduma hiyo lakini kudhibiti wafanyabiashara wenye nia ovu kwa wananchi, pia sheria imeweka kiwango cha mtaji kwa wakopeshaji ili kusajiliwa, lengo likiwa ni kusaidia vikundi vya kuweka na kukopa kuwa na uwezo wa kutoa huduma wakati inahitajika.

No comments:

Post a Comment

Pages