August 12, 2020

Waandishi washauriwa kuandika umuhimu wa USMJ

Mhariri wa Makala wa Gazeti la Habari Leo, Hamisi Kibari akichangia katika mafunzo ya waandishi wa habari yaliyoandaliwa na TFCG na MJUMITA mjini Morogoro.

Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbaliwakiwa katika mafunzo yaliyoandaliwa na TFCG na MJUMITA mjini Morogoro.
Ofisa Sera na Majadiliano wa MJUMITA, Elida Fundi akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini waliokutana mjini Morogoro.
Majadiliano.
Ofisa Uhusiano wa TFCG Bettie Luwuge akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini waliokutana mjini Morogoro.

Waandishi wa Habari wa Vyombo mbalimbali wakiwa na maofisa wa TFCG na Mjumita nje ya ukumbi wa Hoteli ya Edema mjini Morogoro.


Na Suleiman Msuya

WAANDISHI wa habari nchini wameshauriwa kuandika kwa kina habari kuhusu umuhimu na faida Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ) kiuchumi, kijamii na maendeleo.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG), Emmanuel Lyimo, wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali mkoani Morogoro.

Lyimo alisema sekta ya misitu imekuwa na mchango mkubwa kwa jamii ambazo zinazingatia dhana ya USMJ, lakini bado taarifa sahihi hazijafikia kundi kubwa hapa nchini.

Alisema vyombo vya habari na waandishi wakiandika kwa kina habari za uhifadhi wa misitu na faida za kiuchumi, kijamii na maendeleo ambazo zimepatikana zitasaidia jamii kubwa kuelewa.

Mkurugenzi huyo alisema TFCG na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) kupitia Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ua Mkaa Tanzania (TTCS) chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswiss (SDC) wamefanikiwa kuchochea mabadiliko makubwa ya kijamii, kiuchumi na maendeleo katika vijijini 35.

"Tunatoa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari ili kuwajengea uwezo wakuandika kwa kina namna uhifadhi ulivyo na faida za kiuchumi, kijamii na maendeleo pale misingi muhimu inavyoguatwa," alisema.

Alisema rasilimali misitu inaweza kuonekana umuhimu wake iwapo jamii inayozunguka itanufaika na waandishi wa habari ndio watu wa kuonesha matokeo chanya.

Lyimo alisema ipo dhana kuwa ukataji misitu kwa ajili ya mkaa ndio sababu ya uharibifu lakini ukweli shughuli za kilimo ndio chanzo kikuu cha uharibifu na hilo linaweza kuoneshwa na waandishi wa habari.

Alisema TFCG na MJUMITA wameendelea kutoa elimu kwa wananchi namna ya kutumia rasilimali misitu bila kuharibu mazingira huku uendelevu ukidumu.

Mkurugenzi huyo alisema baada ya miaka takribani nane ya kuwajengea uwezo vijiji takribani 35 kwa sasa wanajikita katika ngazi ya wilaya ili ziweze kusambaza dhana hiyo muhimu katika uhifadhi.

Ofisa Mahusiano wa TFCG, Bettie Luwuge alisema kwa sasa wanatekeleza Mradi wa Kuhifadhi Misitu kwa Kuwezesha Biashara Endelevu ya Mazao ya Misitu Tanzania (CoForEST) ambao utahusisha wilaya saba.

Luwuge alisema mafunzo hayo kwa waandishi wa habari yamejikita katika kupeana uzoefu namna ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira na misitu.

"Mradi huu wa CoForEST ni mwendelezo wa mradi wa TTCS, ila tofauti yake ni huu wa sasa unajikita kuendeleza USMJ kwa kushirikisha sekta zote kwa maslahi ya uhifadhi," alisema.

Alitaja wilaya ambazo zitanufaika na mradi huo mpya ni Kilolo, Nachingwea, Ruangwa, Liwale, Morogoro, Kilosa na Mvomero.

Kwa upande wake Ofisa Sera na Majadiliano wa MJUMITA, Elida Fundi alisema pia mafunzo hayo yanawajengea uwezo waandishi namna ya kubaini changamoto zilizopo katika vijiji vya mradi na kuja na mapendekezo.

Fundi alisema uhifadhi wa misitu endelevu unahitaji kila mdau kushiriki hivyo imani yao ni kupitia kundi hilo la waandishi ujumbe utafika kwa usahihi.

Alisema takwimu zinaonesha uharibu wa misitu na mazingira unaendelea kwa kasi hivyo elimu inapaswa kutolewa kwa wadau wote ili kuokoa rasilimali hiyo muhimu kwa viumbe hai.

"Takwimu zinaonesha kwa mwaka hekta 469,000 zinapotea hii ni sawa na Kisiwa cha Unguja sio jambo la kufumbia macho hivyo imani yetu waandishi wakipata ufahamu kila jambo linakuwa sasa," alisema.

a Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA),

No comments:

Post a Comment

Pages