August 17, 2020

Wafanyabiashara wahimizwa kujiunga mtandao wa wateja wakubwa wa Benki ya NMB

Benki ya NMB imewahimiza wafanyabiashara nchini kujiunga na Mtandao wa wateja wakubwa (NMB Business Executive Network) kujua na kunufaika na fursa za elimu juu ya mpangilio na uendeshaji biashara, kodi na taratibu za Serikali kuhusu biashara.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mh. Angelina Mabula akisalimiana na Afisa Mkuuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB - Filbert Mponzi. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Severine Lalika.


Akizungumza jijini Mwanza juzi katika wa mkutano wa mtandao huo wa Kanda ya Ziwa, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB -  Filbert Mponzi alisema wafanyabiashara wanaojiunga na mtandao huo pia hupata fursa kukutana na kujadiliana ana kwa ana na uongozi wa juu wa benki hiyo.


 “Kupitia vikao vya kila mwaka vya NMB Business Executive Network wafanyabishara hupata elimu kutoka kwa wataalam wa fani mbalimbali kuhusu namna bora ya kufanya biashara kirahisi, kwa tija na gharama nafuu kupitia teknolojia,” alisema Mponzi.                          
Sehemu ya wageni waalikwa.


Mtandao huo ulioanza mwaka 2014, tayari unajumuisha wafanyabiashara zaidi ya 760 kutoka miji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya, Kilimanjaro, Mtwara na Morogoro.
“Hata wafanyabiashara wasiyo wateja wa NMB wanaweza kujiunga na mtandao huu kuona fursa, bidhaa na huduma zinazotolewa na benki yetu inayoongoza kwa faida baada ya kodi na ubora kwa miaka 11 mfululizo,” aliongezea Mponzi.


Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa NMB - Alex Mgeni aliwataka wafanyabiashara na Watanzania kwa ujumla kutumia huduma ya bima inayotolewa na benki hiyo ili kupata fidia kwa haraka na wakati kupitia matawi zaidi ya 220 nchini.


“Tayari tumezindua huduma ya bima za aina mbalimbali ikiwemo ya mazao ya kilimo itakayowawezesha wakulima kupata fidia ya madhara na uharibifu unaotkana na majanga kama mafuriko, ukame, uharibifu wa wadudu na ndege waharibifu,” alisema Mgeni.


Naibu wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angelina Mabula aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo aliipongeza benki hiyo kwa kuanzisha bima ya mazao ya kilimo na kuutaka uongozi kuongeza kasi ya elimu kwa umma kuhusu bidhaa na huduma hiyo.


“Bima ya mazao itanufaisha na kuongeza tija katika sekta ya kilimo ambayo mnyororo wake wa thamani unahusisha zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania. NMB endeleeni kuelimisha umma kuhusu huduma na bidhaa,” alisema Dk Mabula.

No comments:

Post a Comment

Pages