August 06, 2020

Wakili Mkuu wa Serikali afunguka hukumu kesi ya mwenendo wa mashauri ya jinai

Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Agosti 6, 2020.


Na Janeth Jovin

Wakili Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata, amesema kuwa ofisi yake haitasita kupeleka rufaa katika mahakama za juu kwa ajili ya kupata nafuu nyingine pindi wanapoona baadhi ya sheria zinakiukwa nchini.

Aidha amesema wanatambua kuwa wanajukumu la kusimamia na kuhakikisha sheria zinasimamiwa na kwamba jamii inajukumu la kuzingatia wajibu na haki zao zinasimamiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu hukumu ya Mahakama ya Rufaa, Wakili Mkuu wa Serikali Malata amesema ofisi yake bado itaendelea kusimamia sheria lakini haitasita kwenda mahakamani pindi takapoona baadhi ya sheria hizo zinakiukwa.

“Tunaiomba jamii itambue kwamba inawajibu wa kuhakikisha sheria zilizopo zinazingatiwa, ofisi yetu itaendelea kuzisimamia na kama tukiona baadhi zinakiukwa hatutasita kupeleka rufaa mahakamani kama tulivyofanya katika shauri la hivi karibuni la Sanga.” Amesema

Hata hivyo amesema  baada ya hukumu kuhusu kifungu cha 148(5) cha sheria ya mwenendo wa mashauri ya jinai kinachozuia dhamana kwa washtakiwa wa mauaji, utakatishaji fedha, uhujumu uchumi na ugaidi kutolewa, wapo baadhi ya mawakili ambao walipinga maamuzi ya mahakama kwamba inashindwa kusimamia katiba.

Aliwaasa mawakili hao kukumbuka wajibu wao bila kujiingiza katika mivutano ya mihimili na endapo hawajaridhishwa na maamuzi wakate rufaa ili wasikilizwe upya na sio kulalamika.

Aliongeza kuwa kama jamii inadai sababu za kupelekwa kwa maombi hayo ni ubambikiziwaji wa kesi, lazima uwepo ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai hayo na kwamba katika kesi hiyo hoja hiyo haijazungumzwa.

“Mahakama kwa kauli moja ilikubaliana na hoja za serikali kwamba kifungu cha 148 (5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai sura ya 20 ya Sheria za Tanzania hakikinzani na Katiba ya nchi,” amesema Malata.

Amesema jopo la majaji watano waliotoa uamuzi katika kesi hiyo ikiwemo Jaji Stella Mugasha, Dk Gerald Ndika, Jacobs Mwambegele, Mwanaisha Kwariko na Ignas Kitusi, lilibainisha kuwa masharti ya kifungu hicho hayakiuki matakwa ya Ibara ya 13 (3) na 15(1) (2) ya katiba.

Kwa kujibu wa hukumu hiyo,  maamuzi ya Mahakama Kuu hayakuwa sahihi kwa sababu katiba ndio inayoruhusu baadhi ya makosa kutokuwa na dhamana.

“Kwa mfano makosa ya mauaji je, ingekuwa watu wanaofanya matendo ya mauaji wanaachwa kwenye jamii wale ndugu wa waliouawa wangefurahi? Na ndio maana Bunge liliamua kuweka sheria hii ili makosa makubwa kama haya ya mauaji na mengine ya uhujumu uchumi, biashara haramu za binadamu, dawa za kulevya na uhaini kutokuwa na dhamana,” amesema Malata na kuongeza;

“Unapoua usitarajie mahakama itakupa dhamana kwani ingeruhusiwa kufanya hivyo, kungekuwa na athari kubwa kwenye jamii ikiwemo usalama wa mtenda kosa anaweza kuuawa, kupoteza mashahidi na pia  itaruhusu kuendelea kwa vitendo vya mauaji katika jamii.”amesema.

Malata alifafanua kuwa masharti yaliyomo katika katiba yanafafanua msingi wa haki, uhuru na uwajibikaji na hayaharamishi sheria sheria iliyotungwa wala kuzuia sheria yoyote kutungwa au jambo lolote kufanywa kwa mujibu wa sheria hiyo.

“Kwa ajili ya kuhakikisha kwamba haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya umma haviathiriwi na matumizi mabaya ya uhuru na haki za watu binafsi, kuhakikisha ulinzi na usalama wa jamii, afya ya jamii, mipango ya maendeleo ya nchi ya kukuza taifa,” amesema.

Pia amesema kifungu hicho kililenga katika kutekeleza vifungu vya 13(3) kuhusu wajibu wa mamlaka nyingine za nchi zinazowajibika kulinda usalama wa raia na mali zao.

Aidha, amesema katiba kama sheria mama inapaswa kutafsiriwa kwa mapana yake kwa kuzingatia malengo, maudhui yake katika kulinda haki ya kila mtu na jamii kwa ujumla na kwamba ikitafsiriwa bila kuhusisha sheria nyingine ni rahisi kuleta sintofahamu katika jamii.

Alisisitiza kuwa utaratibu wa kuzuia dhamana ni wa kikatiba kwani wakati ibara ya 15 (1) ya katiba inampa mtu haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru, ibara ya 15 (2) inaruhusu haki na uhuru wa mtu kuingiliwa kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria lengo ni kulinda haki na usalama wa jamii.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) walikata rufaa hiyo namba 175/2020 wakipinga uamuzi wa Mahakama Kuu katika shauri namba 29/2019 lililofunguliwa na Dickson Sanga akitaka makosa hayo yawe na dhamana kwa sababu kifungu kilichokuwa kinazuia dhamana, kinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Pages