August 05, 2020

WAKULIMA WASHAURIWA KUTUMIA BUNDI KUDHIBITI PANYA MASHAMBANI



Na Mariam Mwayela

WAKULIMA wameshauriwa kutumia ndege aina ya bundi ili kukabiliana na wanyama wadogo pamoja na wadudu waharibifu wa mazao shambani.

Akizungumza wakati wa Maonesho ya NaneNane Dkt.GeorgiesMgode, Mtafiti kutoka Kituo cha Kudhibiti Viumbe Hai Waharibifu katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)amesema tofauti na imani iliyojengeka kwa wengi kuhusu ndege aina ya bundi kuwa anatumika katika shughuli za kishirikina bundi akitumiwa vizuri ana weza kuwa mkombozi wa wakulima kwa kusaidia kupunguza panya na wadudu waharibifu wanaoharibu mazao shambani.

“Bundi ana uwezo mkubwa wa kuona wakati wa usiku hivyo huwinda wanyama wadogowadogo kama panya, wadudu na hata ndege”, alisema Dkt. Mgode.

Dkt. Mgode aliongeza kuwa bundi wanapenda kula panya hivyo wanapokuwa mashambani kwa wingi wanapunguza kwa kiasi kikubwa wingi wa panya ambapo kwa siku moja bundi anauwezo wa kula wastani wa panya kumi na mbili (12).

“Baadhi ya aina za bundi huishi kwa makundi na kuwinda kwa makundi kwa pamoja hivyo ndani ya msimu mmoja kundi moja la bundi linaweza kula mamia ya panya wadogo kwa hiyo bundi wanaweza kudhibiti panya kirahisi na kumsaidia mkulima kupunguza matumizi ya kemikali mashambani”, alisema Dkt. Mgode.

Akielezea kuhusu namna ya kuwafanya bundi wavutiwe na kuzaana kwa wingi Dkt. Mgode alisema kuwa bundi wanahitaji kutengenezewa mazingira mazuri kama vile kujengewa viota kwa ajili ya kuishi na nguzo kwa ajili ya kusimama nyakati za usiku wanapokuwa wanawinda.

“Viota vinaweza kutengenezwa mithili ya masanduku na kuning’inizwa kwenye miti au nguzo lakini mahali ambapo pana miti ya kutosha hapana haja ya kutengeneza viota”, alisema Dkt. Mgode.

Bundi ni aina ya ndege ambaye hula nyama na hufanya mawindo wakati wa usiku na kupumzika wakati wa mchana. Kuna takribani aina 200 za Bundi ambapo wengi wao hupenda kuishi peke yao na kutafuta chakula ambapo huwinda wanyama wadogowadogo kama panya, wadudu na hata ndege.

No comments:

Post a Comment

Pages