August 31, 2020

WARASIMISHAJI ARDHI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI

Baadhi ya Vigingi (Beacons) zilizohifadhiwa ndani katika mtaa wa Engosowashi, Kata ya Moshono mkoani Arusha badala ya kuchimbiwa ardhini kuonesha mipaka ya kiwanja.


 Na Mwandishi Wetu, Arusha

 
KIONGOZI  wa kikosi kazi maalum kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kilichoundwa kwa ajili ya kukwamua changamoto za urasimishaji mkoani Arusha, PrayGod Shao amewataka wanaofanya kazi za upangaji na upimaji makazi holela kuzingatia weleti.


Pia amewataka kuzingatia maadili ya taaluma zao ili kazi zao zikidhi vigezo vya upangaji na upimaji vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria.


Ameyatoa maagizo hayo  Agasti 29, mwaka huu  mkoani Arusha wakati akikagua  kazi za upimaji na uwekaji vigingi (beacons), pamoja na uandaaji wa ramani za upimaji (survey plan), katika mitaa ya Engosowashi Kata ya Moshono na Mtaa wa Olmokea Kata ya Sinoni Shao  amesema  amegundua warasimishaji wengi hawafuati sheria na kanuni za upimaji kwani badala ya kupanda vigingi kwenye mipaka ya viwanja wamevikusanya na kuvifungia ndani ya nyumba kitu ambacho ni kinyume na sheria ya upimaji.


"Vigingi (beacons) vinatakiwa vichimbiwe chini ardhini ili vitumike kama alama ya kubainisha mpaka wa kiwanja kimoja na kingine na siyo kuhifadhiwa ndani," amesema Shao.


Aidha, Shao ameongeza kwamba, mbali na kuvifungia ndani vigingi walivyopaswa kuvichimbia ardhini, bado wameweka alama hewa za upimaji kwenye ramani (Survey plan) ambapo utakuta ramani inaonesha kiwanja kimewekewa vigingi ila ukifika kwenye kiwanja husika hakuna uhalisia
wa vigingi hivyo.
 

Amesisitiza kwamba, serikali kupitia Wizara yenye dhamana ya kusimamia ardhi haiwezi kufumbia macho udanganyifu kama huo unaofanywa na warasimishaji wa kuweka alama hewa za upimaji katika viwanja kwa sababu mwisho utasababisha migogoro isiyo ya lazima.


Shao amesema ni lazima sheria na miongozo ya upimaji izingatiwe kwa kuhakikisha kila kiwanja kiwekewe vigingi vyake na ramani inasomeka vivyo hivyo.


Kwa upande wake msimamizi wa Kampuni ya Savei Consult moja kati ya Kampuni zinazofanya urasimishaji katika mkoa wa Arusha Bryson Michael amesema, uwekaji vigingi (beacons) kwenye mitaa yote ya urasimishaji unasua sua kutokana na mwitikio mdogo wa wananchi wa kulipa gharama za
upimaji kiasi cha Tsh. 150,000 kilichowekwa na Serikali.


Bryson amesema, kazi ya utambuzi wa makazi katika mitaa mitatu kwenye Kata ya Moshono aliyopewa kurasimisha imeshafanyika ambapo michoro ya mipangomiji kwa mitaa hiyo imeshaandaliwa na hivyo upimaji unaendelea.


Kwa kuona umuhimu wa kazi ya urasimishaji mkoani Arusha, Wizara ya Ardhi iliunda kikosi kazi maalum cha kufuatilia na kukwamua changamoto za urasimishaji, na kilianza kazi tangu Agosti 17, mwaka 2020 ambapo kufikia Agosti 30, mwaka huu 2020 makampuni yote yaliyokuwa yanafanya urasimishaji katika Mkoa wa Arusha yanapaswa kukamilisha kazi zao
zote.

No comments:

Post a Comment

Pages