August 05, 2020

WAZIRI KAMWELEWE AITAKA TANROADS KUTIMIZA WAJIBU

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, ameutaka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kutimiza wajibu wao pasipo kusubiri au kusukumwa na maelekezo.

Waziri Kamwelwe alitoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano wa kumi na nne (14) wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala huo nchi nzima uliofanyika mkoani Ruvuma ambapo alisisitiza umuhimu wa kila mtu kwa nafasi yake kutimiza wajibu wake wa msingi katika eneo lake la kazi.

"Tunafahamu changamoto mbalimbali zinazowakabili katika kutekeleza majukumu yenu lakini niwatie moyo na muendelee kuchapa kazi kwa moyo wa kizalendo na kutanguliza maslahi mapana ya Taifa na kuhakikisha hakuna jambo lolote linaloweza kukwamisha ama kuzuia utekelezaji wa majukumu yenu", alisisitiza Waziri Kamwelwe.

Aidha, amewataka kuendelea kusimamia vizuri utekelezaji wa miradi mikubwa inayoendelea hapa nchini hasa ile iliyosainiwa hivi karibuni ikiwemo ujenzi wa barabara ya mzunguko wa jiji la Dodoma, Daraja la Kigongo - Busisi mkoani Mwanza, barabara ya Tanga - Pangani pamoja na miradi mingineyo.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi Waziri Kamwelwe, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye ni Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale, amesema kuwa Wakala unaendelea na utaratibu wa kuweka alama mpya za barabara kuu na za mikoa zinazohitajika na kuboresha zile zilizopo ambazo hazikidhi vigezo kwa mujibu wa sheria.

Mhandisi Mfugale, ameongeza kuwa wakala unaendelea kukemea na kuchukua hatua stahiki dhidi ya vitendo vya utovu wa nidhamu na rushwa katika mizani na unaendelea na mikakati mbalimbali ya kupambana na rushwa katika mizani na kutoa elimu zaidi ya uadilifu ili kubadilisha mienendo mibaya ya wafanyakazi husika.

Halikadhalika, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mheshimiwa Christina Mndeme, ameupongeza wakala huo kwa usimamizi wa miradi ya miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege na kusisitiza kuongeza chachu ya kuendelea kufanya kazi kwa weledi na uzalendo wa hali juu daima.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya TANROADS, Dkt. Dalmas Nyaoro, amemuahidi Waziri Kamwelwe, kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu, bidii, na kuzingatia thamani ya fedha katika miradi yote inayotekelezwa na wakala huo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akihutubia viongozi na wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa Wakala wa Barabara (TANROADS), wakati akifungua mkutano wa kumi na nne wa baraza hilo uliofanyika mkoani Ruvuma.

No comments:

Post a Comment

Pages