September 13, 2020

AGUSTINO SULE, FAILUNA MATANGA VINARA NMB BIMA MARATHON 2020

 

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi hundi ya sh. Milioni 100 Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Lawrence Maseru, (kushoto) wakati alipohitimisha  Mbio za NMB Marathon kwenye viwanja vya Mlimani City jijini Dar es Salaam, Septemba 12, 2020. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Uwekezaji) Angellah Kairuki, wa tatu kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, wa pili kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Sanlam  East Africa, Julius Magabe na wa tatu kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMB, Dkt.Edwin Mhede. Fedha hizo zilizotolewa na Benki ya NMB zitatumika kuwasaidia watoto wenye ugonjwa saratani wanaotibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. 

 

NA MWANDISHI WETU

 

MBIO za NMB Bima Marathon 2020, zimefanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, huku Agustino Sule wa Arusha akiibuka kinara wa nusu marathon (kilomita 21 wanaume), sawa na Failuna Matanga wa Arusha pia, aliyeibuka mshindi wa umbali huo kwa wanawake.

 

NMB Bima Marathon ni mbio zilizogawa nywa katika kategori tano (nusu marathon – kilomita 21, kilomita 10, kilomita 5 na za watoto, ambazo zilizadhaminiwa na Benki ya NMB, zikilenga kutoa elimu ya bima pamoja na kuhamasisha mazoezi ya viungo kwa jamii.

 

Katika kinyang’anyiro hicho kilichovuta hisia za wengi miongoni mwa wakimbiaji nchini, kikianzia na kumalizikia katika Viwanja vya Mlimani City, huku washindi wakikabidhiwa medali na hundi za mfano na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyekuwa mgeni rasmi.

 

Katika kilomita 21 wanaume, Sule aliyekimbia kwa saa 1:05:10), alifuatiwa kwa ukaribu na Nestory Steven wa Singida (1:06:35), huku Faustine Mussa akikimbia kwa saa 1:07:53. Sule alipata kitita cha Sh. Mil. 1, Nestory Sh. 750,000 na Faustine Sh. 500,000.

 

Kwa upande wa wanawake, Failuna aliyetwaa kiasi cha Sh. Mil. 1 za ushindi wa kwanza, alifuatiwa na Nathalia Elisante (zawadi Sh. 750,000), huku nafasi ya tatu ikikamatwa na Sara Iti, aliyejinyakulia kiasi cha Sh. 500,000 za ushindi wa tatu wa mashindano hayo.

 

Gabriel Gerard alikuwa wa kwanza kilomita 10 wanaume, akifuatiwa na Elisante Elibariki na Marco Joseph, huku upande wa wanawake, Grace Jackson akiibuka kinara mbele ya Fadhila Salum na Glory Makula. Washindi walipewa Sh. 700,000, wa pili Sh. 350,000 na wa tatu Sh. 200,000.

 

Katika Kilomita 5 wanaume, Basil Sule, alitwaa ushindi juu ya Meshack Daniel na Paul Masenza, huku kwa wanawake Caterina Moshi aliibuka kidedea mbele ya Amoure Love na Sara Nyello. Washindi kilomita 5 walipewa Sh. 100,000, washindi wa pili 50,000 na wa tatu Sh. 40,000.

 

Katika mbio za watoto za NMB Bima Marathon 2020, Rayan Nuhu aliibuka mshindi akizawadiwa Sh. 100,000, huku akifuatiwa na Juma Laizer (wa pili Sh. 50,000) na Joe Mutunzi (wa tatu Sh. 30,000).

No comments:

Post a Comment

Pages