September 18, 2020

RITA YAJA NA 'ÓNE STOP JAWABU'

 Kaimu Mtendaji Mkuu wa RITA, Emmy Hudson.

 
Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam 


Wakala wa  Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Temeke imeandaa kampeni inayojulikana kwa jina la ‘One stop Jawabu’ maalum kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali ikiwemo vyeti vya kuzaliwa, kuandika wosia,kuandika Mirathi na kutunza sambamba na mambo mengine ya kisheria.


Katika kampeni hiyo ambayo ilizinduliwa rasmi septemba 14 katika viwanja vya Zakhem Mbagala itaendelea kudumu hapo mpaka   septemba 20 kabla ya kuhamia katika viwanja vya Mwembe Yanga Tandika Dar es Salaam.
 

“Tumekuwa hapa tangu tarehe 14 mwezi huu  siku ya uzinduzi tukiwa na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Abubakar Kunenge ambaye alisisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi ili kuweza kutumia fursa hiyo vizuri,’’


“Hata hivyo kuanzia tarehe 22  mpaka 28 mwezi huu tutakuwa katika viwanja vya Mwembe Yanga,Tandika lengo kuendelea kuwafikia zaidi wakazi wa Dar es salaam na ndio maana tunatumia viwanja vya wazi ili waweze kupata huduma hiyo wakiwa kwa wingi,’’alieleza Malema Afisa Habari RITA. 

Pia ofisi ya Mkuu wa wilaya Temeke ambao ndio wadau walioshirikiana na RITA kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa, Godwin Gondwe alisema zoezi kama hilo alilifanya akiwa katika wilaya ya Handeni na alifanikiwa kwa kiasi kikubwa.


“Nililiendesha Handeni kwa kushirikiana na RITA na lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa hivyo nanyi wakazi wa Temeke msilaze damu huduma sasa iko karibu yenu jitokezeni ili mpate huduma mbalimbali za RITA zikiwemo vyeti vya kuzaliwa,’’alieleza Gondwe.


Aliongeza kuwa vyeti vya kuzaliwa vina umuhimu mkubwa hasa katika kuhakikisha unapata cheti cha Utambulisho wa taifa,mikopo vyuoni na hata katika masuala mbalimbali ya ajira.
 

Kwa Mujibu wa Malema mpaka sasa tayari watoto 2700 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa huku zoezi hilo likiwa linaendelea.

No comments:

Post a Comment

Pages