September 03, 2020

SERIKALI YAVITAKA VYUO VIKUU NCHINI KUBORESHA PROGRAMU ZA MASOMO


 Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo, akipata maelezo alipotembelea banda la Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU),  wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.



Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini Profesa Charles Kihampa, akimuonesha Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo, mchoro wa Uwanja Mpya wa soka utakaojengwa jijini Dodoma, wakati alipotembelea banda la Chuo cha Ardhi wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

 


 Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini Profesa Charles Kihampa, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. 

 

Mwenyekiti wa Bodi ya TCU, Prof, Mayunga Nkunya.

 

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo, akitoa hotuba wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

 

Na Mwandishi Wetu

VYUO Vikuu nchini vimetakiwa kuhakikisha vinaanzisha programu za masomo zinazoendana na vipaumbele vya kitaifa hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo.

Dkt. Akwilapo ametoa wito huo Jijini Dar es Salaam wakati leo wa ufunguzi wa maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ambapo amesema kwa kuanzisha program hizo nchi itaongeza ujuzi wa wataalamu lakini pia itaongeza pato la taifa.

Amesema baadhi ya progaramu za kipaumbele kuwa ni mafuta na gesi, afya, hususani udaktari bingwa kwa ngazi za uzamivu katika nyanja zote za magonjwa ya upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, upandikizaji figo, ini na uboho (bone marrow), tiba za ndani za moyo, na uhudumiaji wa wagonjwa wa dharura na mahututi (emergency medicine and critical care).

 “Tusingependa kama nchi kupeleka wagonjwa wetu nchi za nje kutibiwa, bali nchi za nje waje kutafuta tiba kwetu (medical tourism). Kwa kufanya hivyo tutaongeza ujuzi wa wataalam wetu lakini pia tutaongeza pato la taifa,” alisisitiza Dkt Akwilapo.

Akwilapo aliongeza kuwa pamoja na kuanzisha program za vipaumbele nchi kwa sasa inatekeleza miradi mingi mikubwa ambayo inahitaji wasomi wa kuendesha na kusimamia miradi hiyo hivyo ni jukumu la Taasisi za Elimu ya Juu kuhakikisha hili linafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu kwa kuhakikisha wanatoa elimu bora na kwamba  Serikali itaendelea kusomesha kwa wingi Wataalam katika fani na ujuzi adimu na maalum kwa mahitaji ya nchi.

“Ni jambo la kutia moyo kuona kwamba, hivi sasa baadhi ya vyuo vikuu vimeanza kuelekeza jitihada zao katika kutoa elimu ambayo inalenga kushughulikia changamoto za jamii na kuweka msisitizo katika maeneo ya kimkakati ya nchi kama vile Kilimo, Madini, Utalii, Uvuvi, Maliasili na Misitu na Afya,” alisema Dkt Akwilapo  

Aidha amezitaka Taasisi za Elimu ya Juu kuona namna bora ya kupanua udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu kutokana na ongezeko linalosababishwa na udahili wa wanafunzi katika ngazi ya msingi na sekondari na kwamba wanapohitimu lazima wapate nafasi katika vyuo vya kati na vya juu ili kuweza kuwapa ujuzi wa kujiajiri na hivyo kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa Taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu nchini Profesa Mayunga Nkunya  amesema Tume imefanikiwa kuimarisha mfumo wa utoaji ithibati ya mtaala jambo ambalo lilionekana kuwa tatizo kwa muda mrefu na kwamba itaendelea kutekeleza majuku yake ya kuwatumikia watanzania katika sekta ya elimu ili kuhakikisha watanzania katika ngazi zote wanapata elimu bora yenye kukidhi viwango vya ubora kitaifa kikanda na kimataifa.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini Profesa Charles Kihampa amsesama lengo la maonesho ni kutoa fursa kwa vyuo vikuu kujitangaza na kuonesha huduma na kazi wanazofanya na mchango wao katika ustawi wa elimu ya juu kwa mustakabali wa maendeleo ya sayansi teknolojia na manuufaa yake kiuchumi na kijamii. Jumla ya taasisi 67 za elimu ya juu zimeshiriki katika maonesho hayo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliotembelea maonesho 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi ya Teknolojia kwa mwaka 2020 wamesema wamefurahishwa na kuwepo kwa maonesho hayo kwani yanatoa fursa ya kuonana na wahusika na kupata taarifa zinazowawezesha kuomba program zinazoendana na ufaulu wao.

No comments:

Post a Comment

Pages