Washindi wa tuzo ya umahiri wa uandishi wa habari za Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), wenye vyeti wakiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi wa mamlaka hiyo Dk. Agnes Kijazi (wa kwanza kushoto waliokaa), Mwenyekiti wa Bodi Buruhani Nyenzi (katikati waliokaa) na baadhi ya wajumbe wajumbe wa bodi.
Na Irene Mark
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) leo Septemba 7, 2020 imetoa tuzo kwa wanahabari walioandika habari bora za mamlaka hiyo kwa mwaka 2019/2020 na kuleta matokeo chanya kwa jamii.
Tuzo hizo zimehusisha waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari ambao walituma kazi zao kwa TMA ambao walizichakata na kuwapata watatu waliondika habari bora zaidi.
Mwanahabari mshindi wa kwanza ni kwenye tuzo hizo ni Bi. Theopista Nsanzugwanko wa Gazeti la Habari Leo, aliyepata cheti na hundi ya sh. Milioni moja.
Aliyeshika nafasi ya pili ni Jerome Risasi kutoka kituo cha redio na luninga Clouds aliyezawadiwa cheti na hundi ya sh. 700,000 na Daniel Samson mwandishi wa habari kutoka Mtandao wa Nukta alishika nafasi ya tatu na kupata cheti na hundi ya sh. 400,000.
Baada ya kukabidhi tuzo hizo kwa washindi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TMA, Buruhani Nyenzi aliupongeza umoja na ushirikiano uliopo kati ya wanahabari na mamlaka hiyo.
“Miaka michache iliyopita, habari za hali ya hewa ziliwekwa kwenye kurasa za nyuma za magazeti tena kwa ufupi maana yake hazikuonekana kuwa habari muhimu.
“Lakini hivi sasa unakuta habari ya hali ya hewa iko ukurasa wa mbele kabisa tena kubwa haya ni maendeleo makubwa kwenye sekta yetu ya hali ya hewa hongereni sana wanahabari,” alisema Nyenzi.
Alisema umefika wakati sasa taarifa za hali ya hewa kuwa jambo la kuzingatiwa kwa kila sekta na wananchi mmoja mmoja.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agness Kijazi akifungua warsha ya siku moja kwa wanahabari kuhusu maandalizi ya utabiri wa hali ya hewa kwa msimu wa Oktoba, Novemba na Desemba (OND), aliwashukuru wanahabari kwa juhudi za kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa wananchi.
“Mamlaka inatambua juhudi zenu ndio maana hivi sasa matumizi ya taarifa za hali ya hewa yameongezeka... hasa kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu wanasiasa na wananchi wanahitaji sana taarifa zetu ili wajue na wachukue tahadhari kwenye mikutano yao,” alisema Dk. Kijazi.
No comments:
Post a Comment