September 01, 2020

WALIMU 100 NCHINI KUFUNDISHWA MBINU ZA KUFUNDISHIA LUGHA YA KIFARANSA

 

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo (wa pili kulia), akizungumza na Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier, wakati wa kuingia makubaliano ya kutoa mafunzo ya mbinu za kufundisha lugha ya kifaransa kwa walimu 100 . Kulia ni Mkurugenzi wa Elimu ya Juu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Kenneth Hosea.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo (kulia), akijadili jambo na Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier (katikati).

Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU),  Prof. Charles Kihampa (katikati) akijadiliana jambo na ofisa wa ubalozi wa Ufaransa nchini wakati wa kuingia makubaliano ya kutoa mafunzo ya mbinu za kufundisha lugha ya kifaransa kwa walimu 100 . Kushoto ni Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Kenneth Hosea.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo (kushoto waliokaa), Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier (katikati) na Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania,  Prof. Charles Kihampa (wa pili kulia waliosimama) katika picha ya kumbukumbu baada ya kuingia makubaliano ya kutoa mafunzo ya mbinu za kufundishia lugha ya Kifaransa kwa walimu 100 nchini.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk.  Leonard Akwilapo, akiagana na balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier, katika za Ofisi za Wizara ya Elimu jijini Dar Es salaam baada ya kuingia makubaliano ya kutoa mafunzo ya mbinu za kufundisha lugha ya kifaransa kwa walimu 100.

 

NA MWANDISHI WETU

Serikali za Tanzania na Ufaransa zimeingia makubaliano ya kutoa mafunzo ya mbinu za kufundishia lugha ya Kifaransa kwa walimu 100 nchini ambao watakuwa na uwezo wa kufundisha wanafunzi 5,000 wa Kitanzania katika ngazi ya sekondari.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kati ya Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Frederic Clavier na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo kilichofanyika Jijini Dar es Salaam ambapo jumla ya Dola za Kimarekani 250,000 zitatumika ili kufanikisha mpango huo.

Katika kikao hicho wamekubaliana kufanyika kwa vikao vya kitaalamu kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Kituo cha Ubalozi wa Ufaransa (Alliance Francais) ili kupanga utekelezaji wa mafunzo haya ya walimu.

 Aidha, Balozi Clavier ameonesha ameeleza uwepo wa fursa za Watanzania kusoma programu zisizopungua 2,000 za Kiingereza nchini Ufaransa. Ameelezea kuwa  Ufaransa inaandaa Maonesho ya Elimu ya Juu (Higher Education Fair) yatakayofanyika nchini Mei 2021 ambapo vyuo  20 vya Ufaransa vitashiriki kutafuta ushirikiano na Vyuo Vikuu vya Tanzania na Sekta binafsi.

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu Akwilapo ameushukuru Ubalozi wa Ufaransa kwa kuendeleza ushirikiano katika kukuza na kuimarisha elimu ya Juu nchini kupitia ufadhili wa masomo hayo na kuagiza wahusika katika Wizara anayoisimamia kuhakikisha vikao vya kitaaluma vinafanyika ili mafunzo hayo yaweze kuanza kwa wakati uliopangwa.

Katibu Mkuu Akwilapo pia ameahidi kuweka wazi kwa Watanzania kuhusu uwepo wa fursa hizo za  kusoma programu za Kiingereza nchini Ufaransa ili Watanzania waweze kuchangamkia fursa hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages