October 05, 2020

Mtaala wa ualimu ngazi ya cheti kwa elimu ya awali, msingi wafutwa

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikali, Sylivia Lupembe, akizungumza kabla ya kumkaribisha  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Ave Maria Semakafu (katikati), kuzungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Oktoba 5, 2020. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa TIE, Dk. Aneth Komba.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Ave Maria Semakafu (katikati), akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Oktoba 5, 2020 kuhusu kufutwa kwa mtaala wa ualimu wa ngazi ya cheti kwa elimu ya awali na msingi ikwa ni hatua ya kuboresha elimu nchini.
Waandishi wa habari wakifuatilia mkutano huo.
Mkurugenzi Mkuu wa TIE, Dk. Aneth Komba, akizungumza na waandishi wa habari.
 

NA MWANDISHI WETU


WIZARA  ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefuta mtaala wa ualimu wa ngazi ya cheti kwa elimu ya awali na msingi ikwa ni hatua ya kuboresha elimu nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Ave Maria Semakafu, amesema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya kufanyia kazi maoni ya wadau ambao wamekuwa wakiyatoa likiwemo la kufuta mtaala huo.

Amesema mtaala ulioboreshwa unatoa nafasi kwa mwalimu katika mwaka wa pili wa masomo kuchagua eneo la umahiri atakalobobea tofauti na mfumo wa zamani ambao haukuwa katika muktadha huo.

"Mtaala huu mpya utaanza kutumika katika mwaka wa masomo 2020/21 na kwamba mwalimu yeyote mwenye cheti cha ualimu atakuwa na sifa ya kusomea Diploma ya ualimu wa elimu ya awali au msingi na vilevile atakapohitimu na kufaulu atakuwa na sifa ya kujiunga na Chuo Kikuu kupata Shahada ya kwanza ya ualimu wa elimu ya awali au msingi," amesema

Amesema programu itakayofundishwa itakuwa ya miaka mitatu na kwamba masomo yatafundishwa kwa lugha mbili ambazo ni Kiingereza na Kiswahili kutokana na kuwepo kwa shule za English medium nchini.

"Walimu waliosoma Astashada (cheti) bado Serikali inatambua Uhitimu wa cheti katika kada ya ualimu na ipo kwenye mfumo wa utumishi na itaendelea kuwepo na hakuna
mwalimu atakayefukuzwa kazi kwa kuwa yeye ni mwalimu wa ngazi ya cheti," amesema

Amesema kwa walimu walioko kazini watakaopenda kujiendeleza wanaweza kusoma kwa masafa kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania(TIE) kwa njia ya masafa, njia ambayo haita athiri utendaji na mwisho kufanya mitihani ili kupata Diploma.

Dk. Semakafu amesema kwa walimu ambao wana vyeti na hawajaweza kupata fursa ya ajira, watatakiwa kurudi vyuoni na kuweza kupata Diploma ya ualimu.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TIE, Dk. Aneth Komba amesema waboresha mtaala huo ili kuweza kumuongezea hadhi mwalimu na kada ya ualimu kwa ujumla.

"Kwa sasa tutakuwa na Diploma ambayo itamuwezesha mwalimu huyo kwenda kuchua degree ngazi ya elimu ya msingi, hapo zamani tulikuwa hatuna hii degree na ilikuwa kwamba mwalimu akienda chuo Kikuu anatafuta degree ya kufundisha Sekondari na kwa sababu hiyo ilisababisha walimu wengi kuhama  kutoka kwenye ufundishaji wa shule ya msingi kwenda Sekondari," amesema

No comments:

Post a Comment

Pages