Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa Dk. Donald Mmari.
NA MWANDISHI WETU
Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umaskini (Repoa) imesema kuwa itaendelea kuwajengea uwezo watafiti mbalimbali wa hapa nchini ili waweze kufanya tafiti bora na zenye tija kwa jamii na Serikali kwa ujumla.
Aidha Repoa imeishauri serikali kutilia mkazo na kuongeza rasilimali fedha kwenye tafiti ili taasisi na vyuo vikuu vijikite kwenye kufanya kazi hiyo kwa ufanisi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguaji wa semina ya siku mbili kwa waandishi wa habari iliyoandaliwa na taasisi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa Dk. Donald Mmari amesema moja ya mafanikio waliyoyapata ni kuendelea kuwajengea uwezo watafiti.
Amesema wapo watafiti wengi waliopita kwao ambao kwa sasa ni walimu wa vyuo vikuu huku wengine wakifanya kazi katika mashirika ya kimataifa na Serikalini.
"Kiukweli mchango wa watafiti hawa tuliowajengea uwezo umeonekana na tafiti zao zimesaidia sana katika kufatilia jitihada za Serikali za kupunguza umaskini na kukuza uchumi wa nchi," amesema
Akizungumzia taasisi hiyo kutimiza miaka 25 amesema pamoja na serikali sekta binafsi pia inatakiwa kuwekeza nguvu kubwa kwenye tafiti kwa kuwa ndizo zinazotoa taswira ya uchumi.
Dk Mmari alieleza kuwa katika kipindi cha miaka 25 ambacho Repoa imekuwa ikifanya tafiti, imechangia kwa kiasi kikubwa katika upangaji sera na mikakati ya maendeleo.
“Mchango wetu umechagia sana katika upangaji wa sera na mikakati ya maendeleo. Machapisho yetu yamekuwa yakijadiliwa kwa kina na tumeona mabadiliko ya kisera na kimkakati.
Hapo ndipo tunaposema kwamba tafiti zina muhimu sio tu kwa serikali hata kwa wananchi. Mapendekezo yetu yamekuwa yakifanyiwa kazi,” amesema Dk Mmari.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo taasisi hiyo Ina mpango mkakati uliojikita katika kuongeza juhudi za kujenga uweoz wa kufanya tafiti.
“Vyuo vinafanya tafiti ila inahitaji uzoefu na maarifa katika kufanya tafiti za kisera. Tumejikita katika kuongeza uwezo eneo hilo.Kuongeza kasi ya mafunzo kwa watumiaji wa tafiti wakiwemo watunga sera,” amesema Dk Mmari.
Sanjari na hilo Mkurugenzi mtendaji huyo amesema katika miaka mitano hiyo Repoa itajikita zaidi kwenye kufanya tafiti za kimkakati na kuwajengea uwezo wa watafiti ili waweze kufanya kwa ufanisi tafiti za kisera.
“Tangu tumeanza kufanya kazi mwaka 1995 tumefanikiwa kutekeleza lengo letu la kushughulika na watafiti wa ndani hasa katika eneo la uchambuzi wa sera zinazohusu umaskini, tunaahidi kuongeza jitihada katika eneo hilo na tunajivunia kuona watu waliopitia hapa wanafanya shughuli zao kwenye taasisi mbalimbali zikiwemo za kimataifa,”.
No comments:
Post a Comment