December 10, 2020

Benki ya CRDB yaibuka kinara Tuzo za Umahili wa Uaandaji Taarifa za Fedha za NBAA

Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha Dkt. Charles Mwamwaja, akimkabidhi Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo, tuzo ya mshindi wa kwanza kwa upande wa taasisi za fedha ya uwasilishaji bora wa hesabu kwa mwaka 2018/2019 kwa kutumia viwango vya kimataifa vya kutayarisha hesabu zilizotolewa na NBAA
 
===== ===== =====
 
 BENKI ya CRDB imeibuka kinara katika tuzo zinazotolewa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) kama taasisi ya fedha iliyoongoza kwa kuwasilisha Taarifa ya Fedha bora kwa mwaka 2018/2019 kwa kuzingatia viwango vya kimataifa. 
 
Akikabidhi tuzo hiyo, Dkt. Mwamwaja ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuendelea kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa katika utayarishaji wa taarifa zake za kifedha. Dkt. Mwamaja alisema kuandaa ripoti za mwaka za Mashirika na Taasisi za Umma kwa viwango vya kimataifa kunawapatia wananchi fursa ya kupima ufanisi wa utendaji kazi wa taasisi husika, kuona namna gani yanawajibika ipasavyo katika kutumia rasilimali.
 
“Hongereni sana Benki ya CRDB kwa kuibuka kinara katika upande wa taasisi za fedha, hii inadhirisha ni jinsi gani Benki hii imewekeza katika mifumo ya kisasa ya kutoa huduma kwa wateja lakini pia na kuwezesha kupata taarifa za kiwango,” alisema Dkt. Mwamwaja. 
 
Akizungumzia ushindi huo, Afisa Mkuu wa Fedha Benki ya CRDB, Fredrick Nsekanabo, amesema Benki ya CRDB inatambua umuhimu wa kuandaa taarifa za fedha kupitia mifumo inayozingatia viwango vya kitaifa na kimataifa. Alisema kitendo cha kupata tuzo hiyo kunaifanya benki hiyo kuendelea kuongeza jitihada ili kubaki katika nafasi hiyo. 
 
 “Tumefanya uwekezaji mkubwa katika mifumo ya kidijitali hii ni pamoja na kuboresha mifumo yetu ya kukusanya na kuandaa taarifa. Tumeweza pia kuunganisha mfumo wetu wa utoaji taarifa za fedha na mfumo wa kimataifa wa kuandaa taarifa za fedha (IFRS), hii pia imechangia Benki yetu kuwa bora zaidi,” alisema Nshekanabo.
 
Nshekanabo alibainisha kuwa ushindi huo pia unatokana na Benki hiyo kuwa wa mfumo bora wa uongozi  unaozingatia weledi, uwazi wa taarifa za kifedha, uwajibikaji na kiwango cha juu cha uadilifu wa takwimu.  
 
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA Mr.Pius Maneno, alisema Benki ya CRDB imeibuka kinara baada ya kukidhi vigezo vyote vilivyowekwa na taasisi hiyo kwa zaidi ya asilimia 75.   Kwa mwaka 2019 taasisi 61 zimeshindanishwa katika tuzo hizo za NBA zilizo jumuisha vipengele 13. 

No comments:

Post a Comment

Pages