December 06, 2020

Benki ya CRDB yatenga Sh. Milioni 30 ya Ada ya Shule kwa wateja 20 kupitia Akaunti ya Junior Jumbo

 Mkuu wa Kitengo cha Masoko Benki ya CRDB, Joseline Kamuhanda na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi Benki ya CRDB, Stephen Adili wakizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa promosheni ya "Tumekusoti Ada" kupitia akaunti ya Junior Jumbo inayolenga kuwahamasisha wazazi/ walezi kuwafungulia watoto wao akaunti ya Junior Jumbo na kuwawekea akiba ili kutimiza malengo yao hususan katika elimu. Benki ya CRDB imetenga sh. milioni 30 kama zawadi ya ada kwa wazazi wanaowawekea akiba watoto wao katika promosheni hiyo inayotarajiwa kufikia kilele Desemba 31, 2020.

 

Na Mwandishi Wetu


Dar es Salaam, Desemba 04, 2020 - Benki ya CRDB imezindua promosheni ya “Tumekusoti Ada” ikiwa ni muendelezo wa kampeni ya “Jipe Tano” ambayo inalenga katika kuhamasisha wateja kujenga utamaduni wa kuweka akiba iliyozinduliwa mapema mwezi Oktoba.


Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi Benki ya CRDB, Stephen Adili amesema promosheni hiyo inalenga katika kuwahamasisha
wazazi/ walezi kuwafungulia watoto wao akaunti ya Junior Jumbo na kuwawekea akiba kidogo kidogo ili kuwezesha kufikia malengo yao hususan katika elimu.


Kwa mujibu wa Bw. Adili katika promosheni hii “Tumekusoti Ada” ambayo inatarajiwa kufikia kikomo Desemba 31, 2020, Benki ya CRDB imetenga kiasi cha shilingi milioni 30 kama zawadi ya ada kwa ajili ya watoto 20 ambapo kila mtoto atajishindia shilingi Milion 1.5.


“Lengo la promosheni hii ni kuhamasisha wazazi kujenga utamaduni wa kuwawekea akiba watoto, lakini ili kuleta hamasa zaidi na kuonyesha dhamira yetu katika hili tumetenga shilingi milioni 30 kama zawadi ya ada kwa wazazi ambao watakuwa wakiweka akiba mara kwa mara,” aliongezea Adili.


Adili alisema wazazi wengi wamekuwa wakipata changamoto katika kulipa ada za Watoto kutokana na wengi kutokuwa na utamaduni wa kuweka akiba kwa ajili ya watoto. Hali hiyo imepelekea watoto wengi kuchelewa kurudi shule kuendelea na masomo au kujiunga na shule kwa wanafunzi wapi kutokana na kukosa kwa mahitaji ya msingi ikiwamo ada.


“Tuna akaunti maalum kwa ajili ya kusaidia wateja kuweka akiba kwa ajili ya watoto, na hii si nyengine ni akaunti ya Junior Jumbo, ni akaunti ambayo inafunguliwa kwa vigezo nafuu sana, haina makato yoyote na hutoa faida ya riba kwa mteja,” anasema Adili huku akisisitiza kuwa Benki ya CRDB imejipanga kutoa elimu kwa wazazi ili kuwasaidia kuishi
ndoto za watoto wao kwa kumuwezesha kupata elimu bora.


Kushiriki katika promosheni hiyo ya “Tumekusoti Ada”, mzazi/ mlezi anatakiwa awe amefungulia akaunti ya “Junior Jumbo” mtoto wake na kumuwekea akiba mara kwa mara au kumfundisha kuweka akiba mwenyewe. “Mzazi anaweza kuweka fedha katika akaunti ya Junior Jumbo ya mtoto kwa kutembelea tawi, kwa CRDB Wakala, kwa kuhamisha fedha

kutoka akaunti yake kupitia SimBanking au Internet banking au kutoka mitandao ya simu,” aliongezea Adili huku akibainisha kuwa promosheni hiyo pia inalenga katika kuwafundisha wanafunzi umuhimu wa kujiwekea akiba na masuala mengine ya fedha kupitia sherehe zilizoandaliwa kwa ajili ya watoto katika msimu huu wa sikukuu.


Akielezea mwenendo wa kampeni ya “Jipe Tano” Mkuu wa Kitengo cha Masoko Benki ya CRDB, Joseline Kamuhanda hadi sasa Benki hiyo imeshatoa jumla ya zawadi zinazofikia shilingi milioni 20 kwa washindi zaidi ya wateja 3,000 huku akaunti zaidi ya 50,000 zikiwa zimekwisha funguliwa.


“Tunawashukuru sana wateja na Watanzania kwa ujumla kwa kuendelea kuiamini Benki yao ya CRDB. Mafanikio haya yanaonyesha ni jinsi gani Watanzania wamepata hamasa ya
kujiwekea akiba kupitia kampeni hii ya Jipe Tano,” alisema Joseline.


Joseline alisema mafanikio hayo ya Jipe Tano pia yametokana na programu ya “Tupo Mtaani Kwako” ambayo inaendeshwa na Benki ya CRDB ikilenga katika kutoa elimu juu ya huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo kwa Watanzania na kusogeza huduma kwa wateja kupitia njia mbadala za utoaji huduma ikiwamo CRDB Wakala, SimBanking, SimAccount na Internet Banking.


“Katika programu hii ya Tupo Mtaani Kwako wafanyakazi wetu wamekuwa wakiwatembelea wateja mtaani kutoa elimu na kuwapa huduma, hadi kufikia sasa tumeshatembelea wilaya 48 katika mikoa 20. Matarajio yetu ni kufika mitaa yote katika wilaya zote nchini,” anasema Joseline.
 

Joseline alitoa rai pia kwa wazazi kutumia elimu inayotolewa na Benki ya CRDB kuwawekea akiba watoto wao kwani itasaidia sana kuweka msingi bora katika elimu. “Huu
ni msimu wa sikukuu wengi wetu huwa tunafanya matumizi bila ya kujali January tunatakiwa kulipa ada pamoja na gharama nyengine za shule za watoto. Tunawahimiza
kuweka akiba kwa ajili ya watoto kupitia akaunti ya Junior Jumbo,” alisema Joseline.

No comments:

Post a Comment

Pages