December 31, 2020

CMSA yaidhinisha hamisho la hisa za Rabobank katika Benki ya NMB

*Hisa 174,500,000 zahamishiwa Arise B.V.

 

Na Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imeidhinisha uhamisho wa hisa zinazomilikiwa na Rabobank ya Uholanzi katika Benki ya NMB kwenda Arise B.V. (Arise).
 
Arise B.V., ambalo ni jukwaa la uwekezaji, ni kampuni ya Kiafrika ya uwekezaji inayoongoza na kufadhiliwa na wawekezaji mahiri. Muungano wa wawekezaji hawa ulianzishwa mwaka 2016 na Mfuko wa Taifa wa Maendeleo wa Norway (Norfund), Benki ya Maendeleo ya Uholanzi (FMO) pamoja na kampuni ya huduma za kifedha ya kimataifa ya Uholanzi – Rabobank. Kwa mantiki hiyo, Rabobank bado ni sehemu ya wamiliki/umiliki wa NMB Bank Plc kupitia Arise.
 
Lengo la Arise ni kuziendeleza taasisi za ndani za fedha na masoko yenye uwezo mkubwa wa kukua, NMB na Tanzania zikiwa miongoni mwa maeneo pendwa ya kiuwekezaji katika nchi za Afrika zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara (SSA) la kampuni hiyo.
 
Kuidhinishwa kwa hamisho la hisa za Rabobank ndani ya Benki ya NMB kutapelekea hisa 174,500,000 ambazo ni sawasawa na asilimia 34.9 ya hisa zote za benki hiyo, kuhamishiwa Arise.
 
Idhinisho la CMSA linakuja baada ya ombi la hamisho la hisa la Rabobank kupata baraka kutoka mamlaka zote husika za kiudhibiti.
 
Akizungumza kuhusu hamisho hilo la hisa, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi Ruth Zaipuna, alisema kuwa “kufanikiwa kukamilika kwa hamisho la hisa ni ushuhuda tosha wa imani ya wawekezaji katika taasisi yetu na nchi kwa ujumla.”
 
Pia aliongeza kusema: “Ushirikiano kati ya Arise na NMB unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kiutendaji, kibiashara, kimuundo na kifedha ukiwa na tija ya muda mrefu kimasoko ambayo itazidi matarajio ya wanahisa.”
 
Ikumbukwe kuwa NMB ni benki kubwa Tanzania kirasilimali kwa mujibu wa matokeo ya shughuli za kifedha za robo ya tatu ya mwaka huu. Rasilimali zake ziliongezeka kwa kuweka rekodi hadi TZS trilioni 7.0 kutoka TZS trilioni 6.1 kipindi kama hicho mwaka 2019.
 
Pia ni benki inayoongoza kwa kutengeneza faida, baada ya kuwa imepata TZS bilioni 145 wakati wa robo ya mwaka iliyoishia Septemba 30, 2020, hili likiwa ni ongezeko la TZS bilioni 82 mwaka 2019.
 
Uwekezaji huu wa muda mrefu wa Arise utasaidia matarajio ya ukuaji wa siku za usoni wa NMB na kuchochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa Tanzania kupitia ongezeko la huduma jumuishi za kifedha, na ukuaji wa sekta za biashara ndogo ndogo, kampuni za kijasiriamali na kilimo.
 
NMB inawashukuru wanahisa wote, washirika wa kimkakati, wateja na wafanyakazi wake kwa kuendelea kuiamini na kuidhamini.

No comments:

Post a Comment

Pages