December 24, 2020

KAGERA KUNUFAIKA NA UMEME WA UHAKIKA - BYABATO


Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato akimsikiliza Msimamizi wa Kituo cha Kupoza Umeme Kibeta Ndg. Samson Kuboja, wakati alipofika Kituoni hapo kufahamu utendaji kazi wake.

 

Serikali kupitia Wizara ya Nishati  inaendelea kuboresha Huduma ya Umeme kwa kununua mitambo mipya zikiwemo Transfoma, pamoja na kusimamia Ujenzi wa Miradi ya Kufua Umeme ya Rusumo na Kikagati, ili kuondokana na adha ya kukatika kwa Umeme Mkoani Kagera, sambamba na kuachana na Umeme wa kununua kutoka Nchi Jirani ya Uganda.


Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Nishati Adv. Stephen Byabato wakati wa ziara take ya kutembelea na Kukagua Vituo  viwili Vya kupoza na kusambaza Umeme Vilivyopo Kibeta Manispaa ya Bukoba, na Kyaka Wilayani Missenyi Mkoani Kagera na Kuridhishwa na Utendaji kazi wa Vituo hivyo, mapema Desemba 23, 2020. 

Akiwa katika Kituo cha kupoza umeme Kibeta, Naibu Waziri wa Nishati ameshuhudia Mitambo mipya na Kisasa iliyojengwa eneo hilo, yenye uwezo wa  kuzalisha  na kusambaza Umeme wa kiasi cha Megawati 16 huku matumizi ya Umeme kwa Wananchi wa Mkoa Kagera kwa Ujumla Ni Megawati 10.2 mpaka 12 kwa Sasa.

Naibu Waziri Byabato amenukuliwa akisema  "..Nimeridhishwa na Utendaji wa Kituo hiki Cha Kupoza Umeme, kazi yao Ni Nzuri ndio maana tunapata Umeme wa Uhakika, ukiacha changamoto ndogo ndogo ambazo, husababishwa na Mambo mbalimbali ikiwemo Hali ya hewa." Amesema Byabato.

Aidha Naibu Waziri wa Nishati Adv. Stephen Byabato ameishukuru Serikali kwa namna ambavyo imeboresha Miundo mbinu madhubuti na ya Kisasa, ambayo imekuwa na mchango Mkubwa wa kuinua Uchumi wa Mkoa Kagera kupitia Viwanda na mengineyo. Mhe. Byabato ameongeza kuwa kwa Sasa Serikali kupitia Wizara ya Nishati, ipo katika Mpango wa  kununua Transfoma nyingine mbili kubwa zitakazokuwa na uwezo wa kuzalisha Umeme  Megawati 60 kila moja, lengo likiwa Ni kwendana na kasi ya Tanzania ya Viwanda, tunapoingia Uchumi wa Kati. 

Naibu Waziri Byabato ameendelea kuwasihi Wananchi kulinda na kutunza Miundo mbinu ya Umeme, kwa Kuzingatia umuhimu wa Nishati hiyo kwa Matumizi ya kila siku, pamoja na kutojaribu kuhujumu Vifaa na Miundo mbinu ya Kuzalisha Umeme kwa kile kinachoitwa kuuza vyuma chakavu, Jambo ambalo husababisha hasara kubwa kwa Taifa.

Wakati huohuo Naibu Waziri Byabato, ametembelea kituo cha kupoza Umeme cha Kyaka, ambacho hupokea Umeme huo kutokea Uganda na kuridhishwa na Utendaji Kazi, na baadae akapata nafasi ya Kusikiliza Wananchi waliojitokeza kuwasilisha Kero zao sugu, ambazo Baadhi zilipatiwa majibu palepale na nyingine zikiendelea kutatuliwa.

Hayo yanajiri wakati jitihada za Ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Rusumo - Ngara, wa Megawati 80 na ule wa Kikagati - Kyerwa Megawati 14 zikiendelea ili kuhakikisha Mkoa Kagera unapata Umeme wake na kuunganishwa katika Gridi ya Taifa, ili kuondokana na Matumizi ya  Umeme kutoka Uganda kama ilivyo Sasa, ambapo Serikali imekuwa ikitumia pesa Nyingi kununua Umeme huo kutoka Nchi Jirani.

No comments:

Post a Comment

Pages