December 07, 2020

Kamisha wa Bima aipongeza Benki ya CRDB kuanzisha huduma ambatanishi ya bima kwa wateja

Wateja sasa kupata mkono wa pole wa kati ya Sh milioni 2 hadi 15 wa matatizo ya msiba na ajali


Kamishna wa Mamlaka ya Bima (TIRA), Dkt. Mussa Juma (kushoto) na Afisa Biashara Mkuu wa Benki ya CRDB, Dkt. Joseph Witts wakizindua rasmi huduma ya bima ambatanishi ya Benki ya CRDB “KAVA Assurance” ambayo inawawezesha wateja wa ndani na nje ya nchi (diaspora) kupata mkono wa pole wa kati ya Sh milioni 2 hadi 15 wa matatizo ya msiba au ajali.
 
 

Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CRDB, Boma Raballa akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma ya bima ambatanishi ya Benki ya CRDB “KAVA Assurance” ambayo inawawezesha wateja wa ndani na nje ya nchi (diaspora) kupata mkono wa pole wa kati ya Sh milioni 2 hadi 15 wa matatizo ya msiba au ajali. Wengine pichani kutoka kulia ni Meneja Mkuu wa Kampuni Tanzu ya Bima ya CRDB Bank Insurance Ltd, Wilson Mnzava, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Bima ya Sanlama Afrika Mashariki, Julius Magabe, Meneja Mwandamizi Wateja Binafsi Benki ya CRDB, Monika Mushi.

 

Dar es Salaam 07 Desemba, 2020 – Kamishna wa Mamlaka ya Bima (TIRA), Dkt.Mussa Juma ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuanzisha huduma ya bima ambatanishi ya maisha ijulikanayo kama “KAVA Assurance” kwa wateja wenye akaunti katika benki hiyo kwa kushirikiana na kampuni ya bima ya Sanlam Tanzania.
 

Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Mussa alisema kuanzishwa kwa huduma hiyo ya bima kwa akaunti za wateja kutaongeza chachu ya matumizi ya huduma za kifedha pamoja na kuongeza uelewa wa huduma za bima kwa Watanzania.


“Huduma hii ya Bima Ambatanishi katika akaunti za wateja imekuja wakati muafaka ambapo Mamlaka ya Bima imejikita katika kuhakikisha Watanzania wote wanafikiwa na huduma za kifedha ikiwamo huduma za bima,” alisema Dkt. Mussa huku akiitaka Benki ya CRDB na Sanlam kujikita katika kutoa elimu kwa wateja ili kuongeza uelewa zaidi.


Akielezea kuhusiana na huduma hiyo KAVA Assurance Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CRDB, Boma Raballa alisema kupitia huduma hiyo wateja zaidi ya milioni 3 wenye akaunti Benki ya CRDB watakuwa wakipata malipo ya gharama za mazishi pindi mteja anapofariki, gharama za usafirishaji mwili pindi mteja anapofariki nje ya nchi na mkono wa pole pale mteja anapopata ajali inayopelekea ulemavu wa maisha.


“Endapo mteja atapa changamoto hizi basi Benki itatoa mkono wa pole kwa ndugu ambapo kwa wateja wa kawaida mteja atapewa kiasi cha shilingi milioni 2, wateja maalum wao ni shilingi milioni 5 na shilingi milioni 15 kwa wanaoishi nje ya nchi (diaspora),” alisema Raballa huku akibainisha kuwa huduma hiyo ni ya kumuongezea mteja Thamani na hakutakuwa na gharama za aina yoyote kwa
wateja.


Kwa mujibu wa Raballa akaunti zote za Benki ya CRDB zitanufaika na huduma hiyo ya KAVA Assurance kuanzia Akaunti ya Akiba, Akaunti ya Watoto “Junior Jumbo”,
Akaunti ya Wanafunzi “Scholar”, Akaunti ya Wanawake “Malkia”, Akaunti ya

Diaspora “Tanzanite”, Akaunti ya Mshahara, Akaunti ya Hundi, Akaunti ya Wakulima “FahariKilimo”, pamoja na akaunti nyengine.


“Kinachotakiwa ni mteja kutumia akaunti yake mara kwa mara kwa maana ya kuweka akiba na kuitumia kufanya miamala mingine ikiwamo ya malipo ya manunuzi ya bidhaa na huduma kupitia huduma za kidijitali kama CRDB Wakala, SimBanking na Internet Banking,” aliongezea Raballa.


Akielezea utayari wa Benki ya CRDB katika kusaidia kusogeza huduma za bima kwa wateja, Meneja Mkuu wa Kampuni Tanzu ya Bima ya CRDB Bank Insurance, Wilson Mnzava alisema pamoja na kuanzisha kwa huduma ya KAVA Assurance, Benki ya CRDB pia ipo mbioni kuingiza huduma ya bima kidijitali ambayo itawawezesha wateja kupata huduma kupitia simu za mkononi na hivyo kuwafikia Watanzania
wengi zaidi.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu kampuni ya Bima ya Sanlam Afrika Masharika, Julius Magabe alisema kampuni yake inaishukuru Benki ya CRDB kwa fursa hiyo ya kutoa huduma kwa wateja wake zaidi ya milioni 3 idadi kubwa zaidi kulinanisha na idadi ya watu katika nchi za Botswana na Namibia.


“Nitoe rai kwa Watanzania wengi zaidi kuchangamkia fursa hii kwa kufungua akaunti katika Benki yao ya CRDB, kwa kufanya hivyo tutawezsha kufikia lengo la Serikali la kufikisha huduma za Bima kwa asilimia 50 ya Watazania,” alisisitiza Magabe.

No comments:

Post a Comment

Pages