December 20, 2020

SMZ KUWASHUGHULIKIA WATAKAOLETA CHOKOCHOKO ZA KUWAGAWA WANANCHI: MAALIM SEIF

 

 

Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na waumini wa dini ya Kislamu mara baada ya kuswali swala ya Ijumaa huko katika Msiki AL Rahma ulioko Bububu Kijichi Zanzibar.


 


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitomvumilia mtu yeyote ambaye ataleta chokochoko za kuwagawa wananchi na kurudisha hasama miongoni mwao.

Amewataka wananchi visiwani Zanzibar kudumisha amani na umoja uliopo na kuwabeza wale wote wanaopinga umoja uliopo nchini Ili kuipatia Zanzibar maendeleo kwa haraka.

Maalim Seif aliyasema hayo alipojumuika kwa pamoja na waumini wa dini ya kiislamu katika ibada ya Swala ya Ijumaa katika Msikiti wa Ar Rahma uliyopo Bububu Kijichi Unguja.

Maalim Seif ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha  ACT Wazalendo alisema wako watu hawaoni raha wakiona wazanzibar wanakuwa kitu kimoja.

Amesema kuwa kuwepo kwa umoja na mashirikiano ya wazanzibar ni jambo la muhimu katika nchi na kuwataka watu waachane na itikadi za mambo ya kisiasa katika masuala ya kusimamia maendeleo yao.

“Kama tukiwa wamoja ni rahisi nchi yetu kupiga hatua kimaendeleo katika nyanja zote na kuwa mfano wa nchi nyingi za Afrika” alieleza Maalim Seif.

Sambamba na hilo Makamu wa Kwanza wa Rais aliwataka wazanzibar kuacha ubaguzi wa rangi au wa kisiasa.

Pia Maalim Seif alisema dhamira ya yeye na Rais wa Zanzibar Dk. Husein Ali Hassan Mwinyi kufanyakazi kwa pamoja ni kuondoa yale madhaifu yote ambayo hupelekea wazanzibar kutofautiana na kuleta chuki miongoni mwao.

“Tumeunda serikali hii ya shirikishi ili hasama na chuki zote zinazosababishwa na uchaguzi zisijirudie tena kwani hazi tija wananchi wetu” alieleza maalim Seif.

Alisema kuwa wazanzibar watakuwa wamoja vitendo vyoote viovu vitakuwa historia pamoja na vurugu zinazotokea katika kipindi cha uchaguzi.

Alisema kuwepo kwa Serikali yenye muundo wa umoja wa kitaifa ni njia moja ya kubaini sababu ya kupata dawa ya kuilinda Zanzibar isirejee tena katika migogoro isio ya lazima.

Maalim Seif alisema wazanzibar wamebahatika pia kupata dini ya kiislamu ambayo katika maeneo mengi inasisitiza umoja miongoni mwa  jamii ya Waslamu kwa wazanzibar asiliimia kubwa ni waumini wa dini hiyo.

“Tumuombe mwenyezi Mungu atulinde na maadui ambao hawapendi umoja wetu” alieleza Maalim Seif.

No comments:

Post a Comment

Pages