April 29, 2021

DARAJA LA KIYEGEYA MBIONI KUKAMILIKA


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho (mwenye tai), akiangalia mihimili mikuu itakayowekwa kwenye daraja la Kiyegeya, mkoani Morogoro, wakati Waziri huyo alipofika darajani hapo kujionea maendeleo yake. (PICHA NA WUU).

 

Serikali imesema inatarajia kukamilisha ujenzi wa daraja la Kiyegeya, mkoani Morogoro, hivi karibuni, ambalo lilibomoka mwezi Machi, mwaka jana kutokana na mvua kubwa zilizokuwa zikinyesha.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo katika mkoa huo, Waziri huyo amesema kuwa ujenzi huo unatekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kwa kushirikiana na Wakandarasi wengine kwa mtindo wa ‘Force Account’.

“Ningependa kuwapongeza TANROADS kwa kazi nzuri walioifanya tena kwa ufanisi mkubwa, hivyo, tunatarajia baada ya miezi michache daraja hili litakamilika ili wananchi waweze kulitumia tena, mapema iwezekanavyo”, amesema Chamuriho.

Aidha, Chamuriho amesema kuwa ametembelea sehemu wanayotengeneza mihimili mikuu ya daraja hilo na kufafanua kuwa katika miezi michache ijayo kazi ya kuinyanyua na kuiweka juu mihimili hiyo itafanyika, na baada ya hapo utafuata ujenzi wa barabara za maungio mbili ambapo moja itakuwa na mita 1000 na nyingine mita 800, upande wa Dodoma na upande wa Morogoro.

Ameongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo lililopo katika barabara ya Morogoro - Dodoma ni muhimu, kwani ndio njia pekee inayounganisha mkoa wa Dar es Salaam, Morogoro  na mikoa ya Kaskazini ya kati na hata kuelekea nchi za jirani za Rwanda, Burundi na Uganda.

Ametoa rai kwa Mameneja wa TANROADS katika mikoa yote nchini kuhakikisha  wanaendelea kukagua madaraja yote ikiwemo kingo zake, pamoja na kukagua mito yote inayoelekea kwenye madaraja hayo na  kuisafisha ili kudhibiti matatizo ya kukatika kwa madaraja.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS, mkoa wa Morogoro, Mhandisi, Kolante Ntije, amesema kuwa ujenzi unaendelea vizuri na mpaka sasa umefika asilimia 58.

“Kama alivyosema Mheshimiwa Waziri, wakati wowote tunatarajia kuweka mihimili hapa juu, na niwahahakishie watumiajia wa barabara hii kuwa hatutachukua muda mrefu kuikamilisha kazi hii”, amesema Mhandisi Ntije.

Daraja hilo ambalo lilibomoka mwezi Machi, mwaka jana na kuleta msukosuko mkubwa na  hivyo kupelekekea Serikali kujenga daraja la muda pembeni yake, linajengwa upya na Serikali, ambapo ujenzi wake unagharimu shilingi Bilioni 6.9.

No comments:

Post a Comment

Pages