April 29, 2021

HakiElimu yatoa suluhisho elimu tuitakayo

 Wadau wa Elimu wakizindua ripoti ya Eimu Tuitakayo.

Mshauri Mwelekezi wa HakiElimu, Dk. Wilbeforce Meena akichangua ripoti.
Mkurugenzi wa Shirika la HakiElimu, Dk. John Kalage, akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Elimu Tuitakayo.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo (kushoto) akizungumza na Mkurugenzi wa HakiElimu Dk. John Kalage.


NA HAPPINESS MNALE


SIKU chache tangu, Rais Samia Suluhu Hassan, kuhutubia Bunge na kutaka kupitiwa upya kwa sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, ili kutoa elimu ujuzi, Shirika la HakiElimu limekuja na mbinu wezeshi kwa mustakabali wa elimu nchini.
HakiElimu imefanya mapitio ya kina ya Sera hiyo na kuzindua ripoti iitwayo Elimu Tunayoitaka.


Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Mkurugenzi wa HakiElimu, Dk. John Kalage, anasema andiko hilo limetokana na  kuwepo malalamiko na maoni juu ya mfumo wa elimu kutokidhi mahitaji ya Taifa.   
“Sera yenye maudhui sahihi na yanayotekelezeka, ni muhimu katika kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata elimu itakayowajengea umahiri unaohitajika katika karne ya 21. 


“Hakuna elimu bora pasipokuwa Sera Bora,  Tangu kupitishwa kwa Sera ya Mwaka 2014  na kuanza kutekelezwa kumekuwa na hoja muhimu miongoni mwa wadau wa elimu kwamba, Sera hii haikidhi mahitaji ya sasa ya elimu na mafunzo katika nchi ambayo inahitaji kuimarisha mageuzi ya kiuchumi, kijamii, kisayansi na kiteknolojia,”anasema.


Akizungumzia ripoti hiyo Dk. Kalage, anasema Elimu Tunayoitaka ni matokeo ya uchambuzi yakinifu wa Sera ya Elimu ya mwaka 2014 pamoja na sera nyingine.


Anasema andiko hilo limebainisha mazuri ya Sera ya 2014 na mapungufu yake ambayo wanatarajia yatazingatiwa wakati wa  kuandaa sera nyingine. 


Kalage anasema nia yao ni kutoa mapendekezo kuhusu mfumo wa elimu ambao utawaandaa Watanzania kuendana na dunia inayobadilika kwa kasi.


Anasema HakiElimu wamekuwa wakisisitiza kuwa elimu sio cheti ila ni uwezo wa kutenda.  

 
Mshauri Mwelekezi wa HakiElimu, Dk. Wilberforce Meena, anasema ripoti hiyo imegusa maeneo 21 ikiwemo elimu ya awali, msingi, sekondari, Mafunzo ya Ufundi Stadi na Ufundi, elimu ya juu.


Dk. Meena anataja baadhi ya mapendekezo ni kuanzishwa kwa Bodi ya Elimu ya Taifa au Tume ya Taifa ya Elimu itakayosimamia mfumo mzima wa elimu.


Pia Shule za msingi za bweni zisipewe kipaumbele, zinawaondoa watoto kwenye malezi ya msingi ya familia kabla ya kufikia hatua ya kupevuka ujana.


Mapendekezo mengine ni Maadili na Tunu za Taifa zipewe uzito unaostahili katika mfumo wote wa elimu. 


Uanzishwe utaratibu endelevu wa wazi na wa kisayansi wa kuaandaa mitaala unaozingatia tafiti na kuongozwa na wataalam na kusimamiwa na kamati ya kitaifa.


Aidha wamependekeza jukumu kuu la Taasisi ya Elimu Tanzania liwe kuandaa mitaala na kuichapisha na sekta binafsi, wataalam wa kitaifa na kimataifa washirikishwe kwenye uandishi wa vitabu, uzalishaji na usambazaji.


Anasema, mitihani isipewe kipaumbele sana ili kupunguza hofu, hali ya kutojiamini, na kujiona bora kwa kuwaruhusu wanafunzi kuonesha kile walichojifunza na vipaji vyao kupitia tathmini endelevu.


Mgeni rasmi Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo, amewapongeza HakiElimu kwa kufanyika kazi na kutoa mapendekezo ya namna ya kutatua changamoto katika sera ya elimu.

No comments:

Post a Comment

Pages