Mkurugenzi Mkuu wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania
(MJUMITA), Rahima Njaidi akizungumza na mwandishi wa habari namna
mtandao huo umeweza kufikia vijiji vingi venye misitu ya asili.
NA SULEIMAN MSUYA, DODOMA
MTANDAO
wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), umesema katika
kipindi miaka mitano ijayo wataongeza wana mtandao ili kuchochea
uhifadhi wa misitu nchini.
Kwa sasa MJUMITA ina wana mtandao takribani 15,000 kwa miaka 20 ya uwepo wake.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa MJUMITA, Rahima Njaidi wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii jijini Dodoma.
Amesema
MJUMITA imeanzishwa mwaka 2000 ambapo wamekuwa wakijihusisha na
usimamizi wa misitu wakiamini ni njia sahihi ya kuifanya iwe endelevu.
Njaidi
amesema hadi sasa wamefikia vijiji 452 katika mikoa 13 na kuwapatia
mafunzo wanavijiji kuhusu dhana ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya
Jamii (USMJ).
Amesema
katika mchakato huo wamekuwa wakipata ushirikiano mzuri kutoka
Serikalini kupitia Idara ya Misitu na Nyuki, Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania (TFS) na wengine hali ambayo leo umewezesha kupata wana mtandao
takribani 15,000.
"Tunajivunia wananchi wanatuelewa na wanajiunga na mtandao hali ambayo inasaidia uhifadhi kuongezeka.
Ila
juhudi za MJUMITA zimewezesha kupata tuzo mwaka 2015 ya UNDP, Tuzo ya
JIDE kutoka kwa Malkia wa Sweden yote hayo ni ushahidi kuwa tunagusa
wananchi kwenye miradi yetu," amesema.
Mkurugenzi huyo amesema MJUMITA imefanikiwa kuweka hekta milioni 1.8 ya misitu ya asili chini ya usimamizi wa wana vijiji.
"Mafanikio
haya yanatusukuma sisi kuongeza vijiji na mikoa mingine hivyo tutatoka
vijiji 452 vilivyopo kwani lengo kuu ni misitu ya Tanzania iwe salama,"
amesema.
Aidha, wakati
umefika kwa Serikali kuacha uzito kwenye kutekeleza Sera, sheria na
mipango iliyopangwa inatekelezwa ili kuilinda na kuiendeleza misitu.
Njaidi
amesema kwa sasa Tanzania ipo kwenye awamu ya pili ya USMJ ambayo
inataka jamii kunufaika na rasilimali misitu hivyo nguvu ielekezwe huko
kuchochea uendelevu wa misitu.
Mkurugenzi
huyo amesema serikali inatakiwa kutambua lengo la wadau kama MJUMITA na
TFCG ni kuchochea maendeleo na huduma za kijamii na sio wao kunufaika.
No comments:
Post a Comment