May 05, 2021

Benki ya NMB yaendesha droo ya 'Bonge la Mpango'

 

Meneja Mwandamizi wa Bima Benki ya NMB, Catherine Joshua akibofya kitufe kumpigia mmoja wa washindi kwenye shindano la 'Bonge la Mpango' droo ya saba iliyofanyika leo Tawi la NMB Mbezi Louis jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Ofisa Mkaguzi toka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Elibariki Sengasenga na Afisa Huduma kwa wateja Benki ya NMB, Neema Kazaviyo (kulia) wakishuhudia.


Meneja Mwandamizi wa Bima Benki ya NMB, Catherine Joshua akizungumza kwenye shindano la 'Bonge la Mpango' droo ya saba iliyofanyika leo Tawi la NMB Mbezi Louis jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Ofisa Mkaguzi toka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Elibariki Sengasenga na Afisa Huduma kwa wateja Benki ya NMB, Neema Kazaviyo (kulia) wakishuhudia.
Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Mbezi Louis, Nestory Mwombeki (kushoto) akizungumza kwenye shindano la 'Bonge la Mpango' droo ya saba iliyofanyika leo tawini hapo. Wa pili kushoto ni Ofisa Mkaguzi toka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Elibariki Sengasenga, Meneja Mwandamizi wa Bima Benki ya NMB, Catherine Joshua na Afisa Huduma kwa wateja Benki ya NMB, Neema Kazaviyo wakiwa kwenye hafla hiyo.
 
 
NA MWANDISHI WETU

WASHINDI 12 wa droo ya saba ya Kampeni ya Weka Akiba na Ushinde 'NMB Bonge la Mpango', inayoendeshwa na Benki ya NMB, wamepatikana leo, wakiwemo wawili waliojinyakulia pikipiki za miguu mitatu aina ya Lifan Cargo.

Droo hiyo imefanyika kwenye Tawi la Mbezi Louis jijini Dar es Salaam, ambako idadi hiyo inafanya jumla ya wateja 82 kunufaika na NMB Bonge la Mpango, wakiwemo 70 waliojinyakukia pesa taslimu (hadi wiki saba) na washindi 14 waliotwaa zawadi ya pikipiki ya miguu mitatu.

 Akizungumza kabla ya kufanyika kwa droo hiyo, Meneja Mwandamizi wa Bima wa Benki ya NMB, Catherine Joshua, amesema hadi sasa wametoa zawadi zenye thamani ya zaidi ya  Sh. Mil. 109, tangu kuanzishwa kwa NMB Bonge la Mpango - kampeni itakayotoa zawadi za Sh. Mil. 550 hadi itakapofikia ukomo.

"NMB Bonge la Mpango ni kampeni inayo hamasisha utamaduni chanya wa uwekaji akiba, ambako washindi 10 kila wiki hujishindia pesa taslimu, pamoja na pikipiki ya Lifan Cargo (mbili kila wiki), sambamba na gari dogo ya mizigo (maarufu Kama Kirikuu) katika droo za kila mwezi.

"Pia, imo zawadi kuu ambayo ni ya gari la kifahari aina ya Toyota Fortuner yenye thamani ya Sh. Mil. 169. Wito wetu kwa wateja wetu ni kuendelea kuweka akiba inayoanzia Sh. 100,000 katika akaunti zao na kwa wasio na akaunti, kufungua na kuweka akiba kuanzia kiasi hicho ili kujiwekea nafasi ya kushinda," alisema Catherine.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Elibariki Sengasenga, aliwahakikishia wateja wa NMB kuwa Bonge la Mpango ni kampeni inayoendeshwa kwa mujibu wa sheria, ikizingatia taratibu zote na kuwataka kushiriki bila hofu, kwani inafanyika chini ya usimamizi wao.

"Niko hapa kwa ajili ya kusimamia droo hii, ambako ni jukumu letu kama Bodi yenye dhamana. Niwahakikishie washiriki kuwa kampeni hii inatoa washindi kwa kufuata taratibu zote, wito wetu kwao ni kuendelea kujiwekea akiba - ambacho ni kigezo kikuu cha kupata nafasi ya kushiriki," alisema Sengasenga.

Katika droo hiyo, waliojinyakukia pesa taslimu (kiasi walichoshinda na matawi yao kwenye mabano) ni: Imelda Christopher Laizer na Annastazia George Lukinga (500,000), Marietta Kashindye Ndanshau (129,391.60), Mary  Tungucha  (300,000), Sawiya Rashid Mtawala ( 407,200 ).

Washindi wengine wa pesa taslimu wa droo ya saba ni: Joyce Massawe Edesi (298,200), Linus William Rwinwa (298,200) Jonas John Dasare (202,300) ,Bernadetha Philipo William  (304,200) na Letinga Matangi Lyama ( 104,933)

Katika droo hiyo, washindi wawili walioshinda pikipiki za Lifan Cargo walikuwa ni  EMMANUEL ENOS MWAVIPA Mkazi wa BARIADI na KIJIWE MISHKAKI.

NMB Bonge la Mpango ni kampeni ya miezi mitatu iliyozinduliwa mapema mwezi wa tatu (Machi) mwaka huu, ambako licha ya kuhamasisha utamaduni chanya wa kuweka akiba, inatumiwa pia na Benki ya NMB kurejesha kwa jamii sehemu ya faida yake ya mwaka. 

No comments:

Post a Comment

Pages