May 11, 2021

TBS YATOA ELIMU YA VIWANGO KWA WANAFUNZI , WANANCHI WILAYANI KILOSA NA MKINGA

Maafisa wa TBS wakitoa elimu kwa wanafunzi wa shule za Sekondari na Msingi Wanafunzi hao waliahidi kuwa mabalozi na kufurahishwa na hatua ya TBS kuona umuhimu wa kuwafikia kwani vita ya bidhaa hafifu ni ya wananchi wote na si TBS pekee.

Mkaguzi wa TBS Bw.Venance Colman akitoa elimu katika stendi ya Horohoro na soko la Duga lililopo wilayani Mkinga Mkoa wa Tanga. Wananchi hao walifurahishwa na kuishukuru TBS kwa kuwafikia na kutoa elimu itakayowasaidia kuokoa fedha na kuepuka madhara yatokanayo na bidhaa hafifu kwa kununua bidhaa zilizokidhi matakwa ya viwango.

************************************

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

WANAFUNZI wa shule za Msingi na Sekondari na wananchi wanaoendesha shughuli zao kwenye maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu, kama stendi, kwenye masoko, minada,magulio katika maeneo mbalimbali ya Wilaya za Kilosa, mkoani Morogoro na Mkinga, mkoani Tanga wamepewa elimu kuhusiana na umuhimu wa kutumia bidhaa zilizothibitishwa ubora na kusajiliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) .

Kampeni hiyo ya elimu kwa umma ilianza kutolewa maeneo mbalimbali ya Wilaya za Kilosa na Mkinga na maofisa wa TBS kuanzia Mei 4 hadi 10, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Afisa Uhusiano wa TBS, Neema Mtemvu, alisema kitu kikubwa ambacho wamekifanya ni kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari juu ya umuhimu wa kutumia bidhaa zilizothibitishwa na kusajiliwa na TBS, ikiwa ni pamoja na kuwapa namba ya mawasiliano kwa ajili ya kupiga bure kuwasiliana na shirika hilo pindi ikitokea wakapata matatizo au changamoto kwenye bidhaa.

Alisema wamefikisha elimu hiyo kwa wanafunzi kwa kutambua kwamba wataenda kuwa mabalozi wazuri kwa wazazi na walezi kuhusiana na umuhimu wa kutumia bidhaa zilizothibitishwa na TBS.

Kwa upande wa maeneo yenye mikusanyiko ya watu, Mtemvu alisema elimu hiyo imetolewa Mkinga katika Stendi ya Hororo na gulio la Duga, huku kwa upande wa Kilosa elimu hiyo ikitolewa Uhindini, Sabasaba na Kimamba.

Kuhusu mwitikio wa wananchi katika maeneo hayo yenye mikusanyiko ya watu, Mtemvu alisema wengi wamefurahishwa na elimu hiyo na wameomba iwe endelevu .

"Wananchi wameshukuru shirika kwa kuona umuhimu wa kuwapatia taarifa hizo kuhusu viwango kwa sababu wamekuwa wakipata changamoto kubwa, lakini walikuwa hawajui wafanyeje.

Lakini kwa sasa na wenyewe wameahidi kuingia kwenye vita ya bidhaa hafifu kwa sababu wana uwezo wa kuwasiliana na TBS, kwani wanajua tupo," alifafanua Mtemvu.

Alisema miongoni mwa mambo walioelimishwa wananchi hao kupitia kampeni hiyo ni pamoja na majukumu ya TBS, umuhimu ya kuangalia tarehe ya mwisho ya matumizi ya bidhaa wanazotaka kununua, ambapo taarifa hizo zinapatikana kwenye vifungashio.

Eneo lingine ambalo wananchi hao walielimishwa ni umuhimu wa wao kununua bidhaa zilizothibitishwa na kusajiliwa na TBS. Mtemvu alitaja baadhi ya faida za kununua bidhaa zilizothibitishwa na shirika hilo kuwa ni pamoja na kulinda afya zao na thamani za fedha zao.

Alisema mtu anaponunua bidhaa ambazo zimethibitishwa na TBS anakuwa na uhakika na bidhaa anazozitumia. Kwa sasa maofisa hao wanaendelea kutoa elimu hiyo wilayani Bagamoyo, mkoani Pwani.

No comments:

Post a Comment

Pages