Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, Rashid Mwaimu akizunguza katika maadhimisho hayo.
Na Lydia Lugakila, Kyerwa
Kutokana na changamoto ya wananchi wilayani Kyerwa mkoani Kagera kutembea umbali mrefu wa takribani kilometa 80 kufuata huduma ya kimahakama katika Wilaya ya Karagwe mahakama hiyo inatarajia kuanza ujenzi wa mahakama ya wilaya mnamo mwezi juni mwaka huu ili kuwaondolea adha wananchi hao.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera Rashid Mwaimu katika maadhimisho ya utoaji wa msaada wa kisheria kwa wanawake na wasichana uliolenga kuwawezesha upatikanaji wa haki kupitia ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kagera kwa kushirikiana na mtandao wa watoa huduma za msaada wa kisheria TANLAP chini ya ufadhili wa shirika la umoja wa mataifa linalohusika na wanawake (UNWOMEN) yaliyofanyika katika uwanja wa parokia ya mabira jimbo Catholic la kayanga.
Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa wananchi katika wilaya ya Kyerwa kwa muda mrefu wamekuwa wakifuata huduma hiyo kutoka wilayani humo hadi wilaya ya Karagwe kwa umbali wa takribani kilometa 80 jambo ambalo huwalazimu wananchi hao kukata tamaa wakati wakifuatilia masuala ya kisheria.
"Hongereni idara ya mahakama kufikiria mpango wa kujenga mahakama ya wilaya hii itasaidia kuwapunguzia adha wananchi katika kupata huduma ya kisheria ya mahakama ndani ya wilaya yetu"alisema mkuu wa wilaya hiyo.
Akieleza changamoto ya ukosaji wa huduma hiyo muhimu hakimu wa mahakama ya wilaya Anajoyce Chrisostom amesema ujenzi wa mahakama hiyo utawasaidia pakubwa wananchi hao kwani changamoto kubwa ni pale inapotokea wakapokea kesi ya jinai yule mlalamikaji hulazimika kulipa nauli ya mtu anayemlalamikia kwa ajili ya kumpeleka mahabusu ambapo kama amekosa mdhamini, tarehe ya kesi ikifika mlalamikaji hulipa tena nauli ya kumrudisha kutoka mahakama ya wilaya ya karagwe ikiwa ni pamoja na kumlipia nauli askari mgambo aliyemsindikiza jambo linalosababisha wananchi hao kupoteza fedha, pamoja na muda na kusababisha kukata tamaa ya kupata huduma hivyo kisheria.
Aidha kwa upande wake msajili msaidizi wa watoa huduma za msaada wa kisheria Mkoani Kagera Issa Mrimi ameitaka jamii mkoani Kagera kujenga mazoea ya kujitokeza na kupeleka kero zao katika vyombo vya kisheria ili kupatiwa ufumbuzi.
Hata hivyo kilele cha maadhimisho ya huduma ya utoaji msaada wa kisheria kwa wananchi wa wilaya ya Kyerwa imeanza mei 21 mwaka huu katika kata ya Mabira na kilele chake ni mei 22, katika kata ya Nkwenda huku kauli mbiu ikiwa ni "mwanamke inuka omba msaada wa kisheria kwa ustawi wa maendeleo yako"
No comments:
Post a Comment