June 05, 2021

FLAVIANA MATATA FOUNDATION YACHANGIA TAULO ZA KIKE 300 KWA TAASISI YA VOYOTA


Mwakilishi wa Flaviana Matata, Kisha Lushaju, akikabidhi taulo hizo za kike kwa Mkurugenzi wa LaKisha Solutions, Naamala Samson kama waratibu kwa niaba ya Taasisi sauti ya  ya vijana Tanzania  ( VOYOTA).


Flaviana Matata.

 

Na Andrew Chale, Dar es Salaam

FLAVIANA Matata Foundation ya Dar es Salaam imeunga na taasisi ya  VOYOTA katika kuunga mkono kampeni ya  kuchangisha taulo za kike kwa kutoa boksi kumi na mbili na nusu (12.5) zenye jumla ya  taulo za kike 300 kwa taasisi ya Voice of Youth Tanzania (VOYOTA).

Taulo hizo za kike zimekabidhiwa na mwakilishi wa Flaviana Matata, Kisha Lushaju kwa Mkurugenzi wa LaKisha Solutions, Naamala Samson kama waratibu kwa niaba ya Taasisi hiyo ya vijana ya VOYOTA.

"Tunatoa taulo hizi za kike ili ziweze kuwanufaisha mabinti 25 wanaotoka kwenye hali duni,  waweze kujisitiri mwaka mzima wanapokuwa kwenye hedhi". Alieleza Bi. Kisha Lusaju.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa LaKisha Solutions, Naamala Samson akipokea taulo hizo kwa niaba ya VOYOTA, aliishukuru Flaviana Matata Foundation kwa msaada huo wa pedi za LAVY.

"Taulo hizi zitasaidia sana wasichana hawa kuwa katika hali ya usafi na kujiamini wawapo shuleni na tunawaomba wadau wengine kujitokeza kuunga mkono kampeni hii inayolenga kufikia mabinti 500".

"Taulo hizi za kike za LAVY zitapelekwa mkoani Morogoro kwenye shule ya Sekondari ya Mgeta. Kampeni hii itaisha ifikapo mwishoni mwa mwezi wa sita mwaka huu." Alisema Naamala.

Aidha, aliomba kwa wadau wengine watakaopenda kuwasilisha mchango wa fedha au taulo za kike, wanakaribishwa.

"Hii ni kampeni maalum ha kusaidia watoto wa kike katika usafi lengo kufikia mabinti 500. Wadau wote wakiwemo wadau wa vyombo vya habari, wasanii, wanamichezo na wanasiasa na viongozi wote pamoja na wa dini tunawakaribisha sana ama kwa kuwasiliana na Waratibu-VOYOTA kupitia namba 0755 427 000". Alimalizia  Naamala.

Taasisi ya VOYOTA yenye makao yake makuu  Jijini Arusha ilianza kampeni hiyo mwezi Mei mwaka huu na kutarajia kufikia tamati mwishoni mwa mwezi huu wa Juni ambapo pia tayari imeshanunua na kukusanya taulo za kike za kutosha mabinti 305.

No comments:

Post a Comment

Pages