June 14, 2021

JUMUIYA ZITAKAZOVUNJA SHERIA KUCHUKULIWA HATUA

 Na Jasmine Shamwepu, Dodoma


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema Serikali itazichukulia hatua kali Jumuiya zote zilizopo chini ya Wizara yake ambazo zitakiuka sheria na taratibu katika kujiendesha.

Akizungumza leo Jijini Dodoma  na  Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo binafsi nchini (TAMONGSCO), Waziri Simbachawene amesema wale ambao wamekuwa na utaratibu wa kuleta vurugu na kuzivuruga Jumuiya, Wizara yake itachukua hatua kali ambapo amedai ikiwezekana hata pingu zitatumika.

Aidha amesema  Jumuiya hizo zilizoanzishwa na  zinazofanya mambo mazuri katika nchi haiwezekani mtu mmoja akaleta  ugumu hivyo Wizara  itachukua hatua za kisheria na mwenye kuchukua hatua hizo ni yeye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.


Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Binafsi nchini (TAMONGSCO), Alfred Luvanda  amesema wanamshukuru Waziri kwa kusimamia zoezi la  uchaguzi  wa kuwapata  viongozi wapya wa Shirikisho hilo  halali ambapo amedai sasa watakuwa na uhuru wa kufanya Mambo yao huku Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo,Youstor Ntungi akieleza Changamoto ya baadhi ya wenye shule kuchukuliwa kama wafanyabiashara kwa kutozwa kodi nyingi wakati wao wapo kwenye lengo la kutoa huduma ya kumsaidia mtoto yoyote wa Mtanzania.


No comments:

Post a Comment

Pages