Meneja Mradi wa TTCS, Charles Leonard, akielezea maofisa habari wa
serikali na sekta binafsi waliotembea kijiji cha Kitunduweta wilayani
Kilosa mkoani Morogoro namna ya kuanda tanuri bora.
Maofisa habari kutoka serikalini na mashirika yasiyo ya kiserikali wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa TFCG na MJUMITA mbele ya ofisi ya kijiji cha Kitunduweta wilayani Kilosa mkoani Morogoro katika ziara ya kujifunza kuhusu TTCS.
Na Suleiman Msuya, Kilosa
MAOFISA
habari kutoka Serikalini na mashirika yasiyo ya Kiserikali wamesema
Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) umetekeleza
dhana ya uendelevu wa misitu ya vijiji na kulinda mazingira nchini.
TTCS
ni Mradi unaotekelezwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania
(TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA)
chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC)
Mradi
huo unatekelezwa kwenye vijiji 30 vya wilaya ya Kilosa, Mvomero na
Morogoro mkoani Morogoro ambapo umelenga Usimamizi Shirikishi wa Misitu
ya Jamii (USMJ) wenye tija kwa jamii husika.
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hii baada ya ziara ya siku moja kwenye Kijiji
cha Kitunduweta wilayani Kilosa maofisa habari hao wamesema mradi huo
unapaswa kuendelezwa nchini kote kwa sababu una manufaa kwa nchi na
wananchi.
Fredick Bano
Ofisa Mawasiliano Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), amesema ziara hiyo amejifunza mambo mengi ambayo yanamatokeo
chanya hivyo ameahidi kuelezea kwa viongozi wenzeka faida za TTCS.
Bano
amesema TTCS imechochea utunzaji mazingira na kuinua kipato cha
wananchi hivyo inapaswa kusambazwa katika vijiji vyote vyenye misitu ya
asili inayofaa kwa shughuli kama zinazofanyika Kitunduweta.
"Ujumbe
wangu kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa TAMISEMI Ummy Mwalimu
kuendelea kuwaasa viongozi wa halmashauri wa kisiasa na kiserikali
kushirikiana na wananchi kutunza misitu na mazingira kwa njia endelevu,"
amesema.
Ofisa huyo
amesema kupitia mafanikio ambayo ameyaona Kitunduweta atatumia nafasi
yake kushawishi uwepo wa bajeti ya kutosha kwenye USMJ.
Kwa
upande wake Ofisa Habari wa Wilaya ya Kilosa Gladis Mapeka amesema
ziara hiyo imempatia mafunzo mazuri ya namna ya kutumia misitu kwa njia
endelevu.
Mapeka amesema amejifunza namna ya kukata mkaa kwa njia endelevu hali ambayo inaendeleza uoto wa asili kwa siku zijazo.
"Mradi huu wa TTCS unapaswa kuendelezwa kwani unafaida za kimazingira, uchumi, huduma za jamii na maendeleo.
Mfano
tumeambiwa kuwa kila mshiriki anapata kiasi fulani mfano tumeshuhudia
ujenzi wa darasa, nyumba ya mwalimu, choo na hhduma nyingine muhimu,"
amesema.
Meneja Masoko wa
Shirika la Kuhifadhi Mpingo na Maendeleo (MCDI), Innocent Kalokola,
amesema ziara hiyo imempatia manufaa mengi na kuomba isambae nchini
kote.
Kalokola amesema
dhana ya uhifadhi endelevu inayotekelezwa Kitunduweta inachochea misitu
kuwa salama kwani miti michache inazalisha mkaa kidogo.
"Huu mradi unapaswa kusambaa. Niombe Serikali na wadau wengine wa kushiriki kuisambaza," amesema.
Kalokola
amesema kinachofanywa na TFCG na MJUMITA katika mradi wa TTCS
kinashabihina na miradi ya MCDI pamoja na kutokuwepo na uchomaji mkaa.
Naye
Ofisa Mazingira na Elimu wa Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) Kanda
ya Kati, Kawa Kafuru amesema shughuli za uhifadhi wa misiti Kitunduweta
zina tija kwa jamii.
Kafuru amesema njia zinazotumika kuvuna misitu ni njia rafiki kwenye msitu jambo ambalo linaweza kusambazwa nchini.
"Wakati
nakuja nilitarajia kuona jangwa lakini kiujumla msitu upo katika hali
salama jambo ambalo linathibitisha dhana ya uendelevu," amesema.
Akizungumzia
dhamira ya kuwapeleka maofisa habari hao kutoka wizara na taasisi
mbalimbali Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo amesema wanaamini
maofisa hao watakuwa mabalozi wazuri kwa viongozi na ofisi zao.
Lyimo
amesema TFCG na MJUMITA kupitia TTCS, wamefanikiwa kubadilisha mtazamo
wa jamii kuhusu kulinda, kutunza na kutumia rasilimali misitu hivyo
wangependa mabadiliko hayo yasambae kila kona ya nchi.
"Misitu
ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya nchi ila inahitaji ushirikiano
kuhakikisha inakuwa endelevu hivyo kupitia maofisa habari hawa dhana hii
ya uendelevu itasambaa," amesema.
Meneja
Mradi wa TTCS, Charles Leonard amesema ili misitu iweze kuwa endelevu
ni lazima jamii inayozunguka iweze kunufaika na mradi huo umeonesha
matunda chanya.
"Tanzania
ina hekta milioni 48.1 za misitu ambapo hekta milioni 22 ni misitu ya
vijiji ila iliyopo kwenye USMJ ni hekta milioni 1.5 hivyo ni wazi nguvu
zinahitajika kuhakikisha hekta zaidi ya milioni 20 zinahifadhiwa kwa
njia endelevu," amesema.
Meneja
huyo amesema takwimu zinaonesha kwa mwaka zaidi hekta 479,000
zinapotea hii ikiwa ni mkoa wa Dar es Salaam mara tatu hivyo ni vema
serikali na wadau kuwekeza kwenye utunzaji na uhifadhi misitu kwa njia
endelevu.
No comments:
Post a Comment