June 22, 2021

MARAHABA MUSIC EXPO 2021, KUFANYIKA BUJUMBURA, BURUNDI

 

Marahaba Band.



NA ANDREW CHALE


TAMASHA kubwa la Muziki la Kimataifa la Marahaba Music Expo ambalo lenye kauli mbiu 'International Music Forum for Africa', msimu wa Pili linatarajiwa kufanyika tarehe 30-31 Julai, Mjini Bujumbura, Burundi huku Wasanii mbalimbali wakitarajiwa kutoa shangwe la nguvu kwenye majukwaa mawili tofauti.

Kwa mujibu wa taarifa ya mtandao wa kijamii wa tamasha hilo wa Facebook, Marahaba Cfestival umeeleza kuwa, tamasha hilo ambalo kwa asilimia 100 ni la mubashara 'live' wanatarajia kuwa na Mwanamuziki wa Kimataifa wa Cameroun, Armand Biyag  na wasanii wengine mbalimbali kutoka mataifa ya Afrika na Ulaya ambao watapeleka shangwe Bujumbura, Burundi.

Ambapo imeelezwa kuwa, katika siku hizo mbili za tamasha, shughuli mbalimbali zitaendeshwa ikiwemo mafunzo ya masoko kwa wanamuziki pamoja na mafunzo ya kutengeneza sauti [Sound engineer] ambayo yatatolewa na wabobezi wa nyanja hiyo.

"Wakati wote wa tamasha kutakuwa na shangwe na shughuli mbalimbali. Shughuli safari hii tumefunga majukwaa mawili tofauti katika mji wa Bujumbura likiwemo jukwaa la Kaskazini [ Northe] na jukwaa  la la pili litakuwa pale eneo la Institut Francais Bujumbura, watu wote watashuhudia hili tamasha bure kabisa".  Ilieleza taarifa hiyo.

Baadhi ya Wasanii na ambao watashiriki mwaka huu ni pamoja na; Armand Biyag  kutoka Taifa la Cameroon, Rally Joe [Burundi], Bernice the Bel [Burundi], Maalem Issam Art [Mali],Eric Pounouss [Reunio], Masterland [Burundi],  na Biglad [Cameroon].

Wasanii wengine ni; Jampara the Bata Lioni kutoka Taifa la Holand, Aglae Aletta [Burundi], Chirba Dia [Senegal],DJ Mbowe [Tanzania], Alwatan Taarab Band [Burundi], Just way [Burundi], Bechou [Burundi], King Etienne [Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-RDC], Gerard Ndikubwayo [Burundi],Marahaba Band [Burundi],Afro talent band [Burundi],

Pia wapo: Club Intatana, Warumba wa Nyakanga, Ruciteme Group, Rukinzo band, Orchestre National Mucowera, Charis Music band na wengine wengi.

Aidha, imeeleza kuwa, tamasha hilo tokea kuanzishwa kwake miaka mitatu iliyopita limekuwa na lengo la kukuza uchumi pamoja na kuleta wasanii pamoja wa ndani na wale wanje katika tamaduni ya muziki kwenye kufikisha jumbe mbalimbali.

"Tuna sehemu zetu za vivutio ikiwemo Mise vivant watu watakaofika hapa hasa wageni watafurahia muziki mzuri na tamaduni lakini pia watatembelea kuona wanyama wa kila aina kwenye hii zoo.

Pamoja na udogo wake wa umri toka tumelianzisha hili tamasha, Burundi hakukuwa na tamasha muda mrefu, hili ndiyo tamasha la kwanza la Kimataifa lililopo kwa sasa na limeorodheshwa katika Matamasha makubwa ya Kimataifa147, Duniani ambapo limekuwa likikuwa kwa kasi." Ilieleza taarifa hiyo.

Wameongeza kuwa, Mbali ya Marahaba Music Expo ambalo linajumuisha Wasanii na  Waandaaji matamasha makubwa ya muziki, pia kila mwaka wanaendesha tamasha dogo la Marahaba  Local music Festival, wakihusisha zaidi Wasanii, vikundi vya muziki pamoja na waandaaji wa muziki wa ndani ya Burundi pekee.

"Tuna Matamasha makuu mawili, Marahaba Local Music Festival lenyewe linafanyika kila mwaka na msimu huu ni mwaka wa tatu tokea kuanzishwa kwake likiwa na lengo la kukuza muziki wa ndani ya Burundi. Lakini tamasha la Pili ni la Marahaba Music Expo lenyewe linahusisha wasanii, vikundi na waandaaji wa matamasha ya muziki wa Kimataifa na wa ndani ambapo hufanyika kila baada ya miaka miwili hivyo mwaka huu linakuwa mwaka wake wa pili" Ilieleza taarifa hiyo.

Iliongeza kuwa, Wamefanya matamasha mawili zaidi ya 'Marahaba'  ilikutoa fursa na pia kupata vionjo tofauti kwenye tasnia hiyo ya muziki.

"Wasanii wetu wa ndani wanapenda sana kwenda nje kuonyesha Sanaa zao na hivyohivyo Wasanii wa nje ama wageni nao wanapenda zaidi kuja kwetu Afrika kuleta Sanaa (muziki wao)  yao hivyo tumerahisisha". Ilisema taarifa hiyo.

Marahaba music Expo imekuwa na lengo la kukutanisha pomoja wadau wa muziki kupata mafunzo na mazungumzo ya wasanii wa Bara la Afrika kutumia muziki wao jukwaani, Semina na maonyesho mbalimb huku  pia uwepo wake unachangia ongezeko la kiuchumi kupitia wageni wanaofika kulishuhudia na kukuza shughuli za Utalii wa Taifa hilo.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment

Pages