Mbegu Bora.
NA BETTY KANGONGA
MABADILIKO ya Tabianchi ni mabadiliko ya hali ya hewa ya muda mrefu katika eneo fulani (Mkoa, Nchi au Bara) tofauti na iliyozoeleka.
Mabadiliko hayo huleta athari katika nyanja za kiuchumi, kimazingira na kijamii. Mabadiliko ya Tabianchi ni tatizo linaloikabili dunia katika karne ya ishirini na moja kutokana na athari zake katika nyanja mbalimbali zinazogusa maisha ya binadamu wa kawaida kila siku ikiwa ni pamoja na kilimo na ufugaji.
Kila mwaka takribani watu milioni 200 duniani wanaathirika na ukame, mafuriko, vimbunga, matetemo, moto na majanga mengine, hivyo kuongeza kasi ya watu kuathirika kiuchumi na kuongeza idadi ya watu masikini duniani.
Kuwepo kwa majanga haya kunatokana na sababu mbalimbali zitokanazo na kuongezeka kwa shughuli za binadamu zinazoathiri mfumo mzima wa hali ya hewa ikiwemo ukataji wa miti, uvuvi usiozingatia utaalamu pamoja na matumizi mabaya ya ardhi.
Tanzania pia imekuwa ikikumbwa na majanga mbalimbali kama ukame, mafuriko, moto, vita vya wakulima na wafugaji na milipuko ya mabomu ambapo majanga yote haya yalileta athari kwa wananchi na mali zao.
Katika mwaka 2013/14, ukame ulisababisha upungufu wa chakula kwa watu 828,063 katika wilaya 54 za mikoa 14 nchini na Serikali ilitoa tani 26,663 za chakula cha msaada chenye thamani ya Sh.Bilioni 2.2 kwa ajili ya kusafirisha chakula hicho kwa walengwa.
Sekta ya Kilimo ni uti wa mgongo kwa wananchi na uchumi wa Tanzania na kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kumechangia kwa kiasi kushuka kwa uzalishaji wa kilimo na kutotabirika kwa mvua kumeathiri wakulima.
Ili kukabiliana na hali hiyo wadau wa kilimo walishauri kuwepo kwa mkakati maalum wa kuhakikisha wakulima wanapatiwa mbinu mbadala kuweza kukabiliana na hali hiyo ikiwa ni pamoja na matumizi ya mbegu bora za kilimo.
Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wananchi na waangalizi wa haki za ardhi vijijini wa Wilaya ya Morogoro wanasema kuwa wamewataka wataalam wa masuala ya mbegu kuwa karibu na wakulima ili kuhakikisha wanalisaidia kundi hilo kuepukana na matumizi ya mbegu zisizo na ubora hasa katika kipindi hiki cha Mabadiliko Tabianchi.
Waangalizi hao wanasema, wakulima walio wengi wanakabiliwa na matumizi ya mbegu zisizo na ubora jambo linalosababisha mavuno duni.
Tatu Maleta wa Kata ya Kisaki Mkoani Morogoro anasema kuwa ni muhimu wataalamu wa masuala ya ugani wakawa karibu na wakulima ili kutokomeza tatizo hilo ambalo limekuwa tishio kwa wakulima.
“Huduma ya ugani ikipatikana kwa ukaribu kuna uwezekano wa kuondokana na matumizi ya mbegu zisizo na ubora ambazo zimekuwa zikiharibu ardhi,” anasema.
Anasema kuwa mabadiliko tabianchi yamewaathiri wakulima wa eneo hilo kwa kuwa kipindi cha kilimo cha mpunga kuliibuka wadudu ambao walishambulia zao hilo hatua iliyosababisha wakulima kukosa mapato.
“Hadi sasa hatujajua aina ya wadudu hao waliokuwa wakishambulia zao hilo ndiyo maana tunahitaji kuona wataalamu wetu wakiwa karibu nasi ili kuondokana na tatizo hilo ambalo limekuwa likisababisha hasara kwa wakulima,” anasema.
Naye Mwangalizi Seleman Puga wa Kisanga, mkoani Morogoro anasema, wataalamu wa kilimo waangalie namna ya kulisaidia Taifa katika kuongeza ubora wa mbegu zetu za asili ili kuepuka matumizi ya mbegu ambazo zinaonekana kuharibu ardhi.
Anasema kuwa utafiti wa mbegu za kilimo unapaswa kufanyika katika maeneo yanayojishughulisha kwa kilimo akitolea mfano Iringa, Arusha na Kilosa ili kubaini aina ya wadudu wanaopatikana katika maeneo hayo.
Naye Samuel Qawoga anasema, kutokana na mabadiliko ya tabianchi baadhi ya wataalamu wamekuwa wakidai kuwa mbegu za asili hazifai hivyo ipo haja ya wakulima kutumia mbegu za kigeni jambo ambalo linahatarisha ardhi zao.
Naye Ramadhan Kibali wa Kijiji cha Kongwa anasema, kuwa wamekuwa wakipambana na wadudu waharibifu wa mazao bila kupata suluhisho huku wakati mwingine wakijaribu kuwasiliana na maofisa kilimo lakini hakuna hatua zinazofanyika zaidi ya kupewa maneno tu.
“Unajaribu kuwasiliana na ofisa kilimo na kumjulisha kuhusu wadudu wanaoshambulia shamba langu lakini nae hana anachonisaidia zaidi ya kunitaka nikamchukue huyo mdudu na kumleta ofisini kwake,
…kisha anakwambia atakupa jibu lakini ukifuatilia hakuna lolote lililofanyika hivyo ninaomba hawa wataalam watusaidie kuondokana na aina ya wadudu waharibifu wa mazao,” anasema.
Naye mwezeshaji wa mada hiyo Fazal Issa anasema, kuwa upungufu wa maofisa ugani nchini imechangia kuwepo kwa matatizo mbalimbali yanayowakabili wakulima, kwa kuwa asilimia 40 hawana vitendea kazi.
KAULI YA OFISA KILIMO
Akizungumzia suala hilo Ofisa Kilimo wa Mazombe mkoani Iringa Jasmin Mtuga anasema, kuna haja ya serikali kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa maofisa ugani ili kuweza kubaini aina ya wadudu waharibifu wa mazao wanaoibuka katika maeneo mbalimbali nchini.
“Ni ukweli kuwa mimi sina kifaa cha kuweza kubaini aina hii ya mdudu mharibifu anapaswa kupuliziwa dawa gani badala yake itanilazimu kuomba msaada kwa wahusika hivyo matokeo yake mkulima kushindwa kupata suluhisho la tatizo lake kwa wakati,” anasema.
Hata hivyo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia kitengo cha Uhawilishaji teknolojia na mahusiano ina mpango wa kuzalisha mbegu za aina mbalimbali kwa ajili ya kuwafikia wakulima na kuwaondoa katika matumizi ya mbegu za zamani ambazo hazina tija kwao.
Tari inasema kuwa zipo mbegu zaidi ya aina 200 za mazao mbalimbali yakiwemo ya mizizi na mafuta ambazo kwa kiasi kikubwa hazizalishwi na ASA licha ya kuwa na kibali cha kuzalisha mbegu zote ili mkulima asikose mbegu kwa maendeleo ya Taifa.
Hata hivyo watafiti waliopo katika vituo 16 vya Utafiti wa mazao mbalimbali nchini yakiwemo ya biashara watumie nafasi ya uhawilishaji waliyonayo kuhakikisha wakulima waliopo kwenye maeneo yanayowazunguka wanalima mazao hayo.
Mkaguzi Mwandamizi wa Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Emmanuel Mwakatobe aliwahi kuzungumza kwenye mdahalo wa haki ya mbegu kwa wakulima wadogo na kusema karibu asilimia kubwa ya wakulima wote waliopo nchini wamekuwa wakitumia mbegu zisizo rasmi kutokana na kukosa elimu ya mbegu bora.
Mabadiliko Tabianchi na matumizi ya mbegu zisizo rasmi yameendelea kusababisha wakulima kukosa mavuno na kushindwa kukidhi haja ya mahitaji ya kifamilia na hata kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Taasisi ya Utafiti na Utetezi wa Haki za Ardhi (HAKIARDHI), imekuwa mstari wa mbele kufanya uchambuzi wa athari za mabadiliko ya tabianchi na haki za ardhi kwa wazalishaji wadogo.
Uchambuzi huo ni pamoja na kuibua namna ambavyo mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri haki za ardhi hususani kwa wazalishaji wadogo ambao hutegemea majira na nyakati za mvua na jua katika kuendesha kilimo pamoja na ufugaji.
Tanzania imeridhia na kutekeleza makubaliano ya kimataifa yenye miongozo ya kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi kulingana na jinsi nchi yetu ilivyobainisha katika mikakati ya kitaifa.
Makubaliano hayo ni pamoja na UNFCCC na Mkataba wa Kyoto wa 1996 na 2002 ili kuhakikisha kuwa masuala ya mabadiliko ya tabia nchi yanaungwa mkono na Sera na Sheria za nchi.
Kupitia Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997, Tanzania imejiwekea mazingira mazuri katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Vilevile, kuna mipango na mikakati inayolenga kukabiliana na mabadiliko hayo, mfano Mkakati wa Mabadiliko ya Tabianchi (2012) ambao unalenga kuiwezesha Tanzania kuhimili na kushiriki katika jitihada za kidunia za kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa mitazamo wa kufikia maendeleo endelevu.
Mipango mingine ni Mpango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (2013) ambao unalenga kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuwezesha ujumuishaji wa namna ya kuhimili mabadiliko katika sera, programu na mipango ya maendeleo.
Hivi karibuni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Selemani Jafo, amezindua Mpango Mkakati wa Taifa wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi mwaka 2021 hadi 2026 huku akiitaka jamii kuishi kwa kufuata misingi ya ajenda za kimazingira.
Jafo anasema, kuwa Mkakati huo utasaidia kuondokana na uharibifu wa mazingira uliopo kwa sasa.
Anasema kuwa kutokana na mapinduzi ya viwanda na shughuli za kibinadamu zimechangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya tabianchi na kuipa changamoto Dunia Katika kutafuta suluhu za kimazingira.
“Bila kulinda mazingira, dunia haitokuwa sehemu salama na uchumi wa mataifa mengi utadidimia hivyo kuna haja kwa nchi zilizoendelea kuzisaidia nchi masikini kupambana na athari za kimazingira, zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi,”anasema.
Anasema kuwa, wataalamu wanaeleza asilimia moja ya pato la Taifa linapotea kila mwaka kutokana na mabadiliko ya tabianchi pia ikikadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 1.6 wa ukanda wa pwani watakabiliwa na changamoto za Mazingira ifikapo mwaka 2030 ikiwa jamii haitaacha shughuli za kibinadamu zinazoathiri mazingira.
No comments:
Post a Comment