June 22, 2021

MGANGA MKUU WA SERIKALI APONGEZA UZINDUZI NMB HEALTHCARE CLUB


Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Ndani Benki ya NMB, Benedicto Baragomwa, akizungumza wakati wa uzinduzi wa 'NMB Healthcare Club,' uliofanyika Dar es Salaam.

 


Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Aifelo Sichwale, akitoa hotuba yake wakati wa uzinduzi wa 'NMB Healthcare Club,' uliofanyika Dar es Salaam.


Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Aifelo Sichwale (kushoto), akipata maelezo kutoka kwa, Elizabeth Lema ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Cornwell Tanzania inayojihusisha na utengenezaji wa dawa za asili na virutubisho, wakati wa uzinduzi wa 'NMB Healthcare Club,' uliofanyika Dar es Salaam jana. Wa pili kutoka kushoto ni Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Ndani Benki ya NMB, Benedicto Baragomwa.


 Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Aifelo Sichwale (wa pili kushoto), akipata maelezo kutoka kwa mwakilishi wa Chama cha Wanasayasi wa Maabara za Afya Tanzania (MELSAT), Godfrey Hongoli (kulia), wakati wa uzinduzi wa 'NMB Healthcare Club,' uliofanyika Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Ndani Benki ya NMB, Benedicto Baragomwa.

 


 NA MWANDISHI WETU


BENKI ya NMB, imekuwa ya kwanza nchini kuzindua 'NMB Healthcare Club,' mtandao unaowapa wadau wa Sekta ya Afya mikopo ya vifaa kazi, mitaji na uwekezaji, huduma inayokuja huku benki hiyo ikiwa imetumia zaidi ya Sh. Bilioni 32 kutoa mikopo kwa Sekta Binafsi ya Afya, kati ya Sh. Bilioni 112.5 ilizopanga kutumia hadi mwaka 2025.

NMB Healthcare Club imezinduliwa sambamba na Kongamano la Afya 'Tanzania Health Summit 2021,' uzinduzi uliowakutanisha wadau wa Sekta ya Afya zaidi ya 150, wakiwemo madaktari, wamafasia, wamiliki wa hospitali, zahanati, vituo na vyuo mbalimbali vya afya na viongozi wa vyama washirika.

Uzinduzi huo umefanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, ambako Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Aifelo Sichwale, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, aliipongeza NMB kwa kuwaunganisha na kuwapa uwezeshaji wadau muhimu wa Sekta ya Afya nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dk. Sichwale alibainisha kuwa, wajibu wa kutoa huduma kwa wananchi, zikiwamo za afya ni wa Serikali, lakini fursa na uwezo havitoshelezi, hivyo kufungua milango kwa Sekta Binafsi ya Afya na kwamba wataendelea kushirikiana na wadau wote wanaohudumu katika sekta hiyo.

"Uzinduzi huu unaofanyika leo una baraka zote za Serikali na tunawaunga mkono NMB kwa juhudi zenu za kuwaunganisha madaktari na wadau wengine muhimu wa Sekta ya Afya hapa nchini, katika kusapoti malengo ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha mazingira ya sekta hii.

"Malengo ya Serikali ni kuboresha mazingira ya wafanyabiashara kushiriki kukuza Uchumi wa Taifa kupitia kodi wanazolipa, kutoa ajira na kuongeza mitaji. Tunaamini kupitia NMB Healthcare Club, wanachama watapata mafunzo kuhusu maarifa ya kibiashara pamoja na elimu kifedha," alisema Dk. Sichwale.

Aliipongeza NMB sio tu kwa kuwaunganisha wadau hao muhimu, bali utayari wao wa kutoa bure elimu ambayo mahali pengine wangeipata kwa gharama kubwa, hasa juu ya uwekaji akiba, uwekezaji, umuhimu wa kupitisha fedha zao kwenye akaunti ya benki, pamoja na huduma zinginezo

Naye Kaimu Afisa Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Benki ya NMB, Benedicto Baragomwa, aliwapongeza wadau wa Sekta ya Afya kwa mapambano katika kipindi cha janga la COVID-19, na kwamba wao kama benki waliwaunga mkono wateja wao kwa kuwapa ahueni za kifedha na kubadili mfumo wa urejeshaji wa mikopo yao. 

"Ukaribu wetu kwa wateja ulilenga kuwawezesha kuhimili changamoto zilizotokana na janga la Corona. Kwa sababu sisi NMB tumekuwa mstari wa mbele katika kusaidia sekta hii ya afya, ambako tunatoa misaada ya vifaa tiba, vikiwamo vinavyolenga kuhudumia eneo lenye changamoto nyingi, la afya ya uzazi.

"NMB tumeingia kwa nguvu moja kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wote, ambapo kupitia huduma ya Asset Financing - inayotoa mikopo nafuu mahsusi kwa Sekta Binafsi ya Afya, tumetumia zaidi ya Sh. Bilioni 32 Hadi Machi mwaka huu, kati ya Sh. Bilioni 112.5 tulizopanga kutumia hadi mwaka 2025.

Kwa upande wake, Rais wa Tanzania Health Summit, ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Phisiolojia Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dk. Omary Chillo, aliiomba Serikali kuongeza nafasi za wadau wa Sekta Binafsi ya Afya kushiriki vikao vya mipango kazi wizarani.

Naye Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Shedrack Mwaibambe, aliitaja NMB kama benki ambayo haijawahi kuacha kujaribu katika kila eneo kuhakikisha inaikwamua Sekta ya Afya Tanzania, na kwamba NMB Healthcare Club ni uthubutu mwingine unaowapa nguvu za ziada wawekezaji na wadau muhimu waliopo katika sekta hiyo.


No comments:

Post a Comment

Pages