June 01, 2021

Mjasiriamali Sinza akabidhiwa Pikipiki ya NMB Bonge la Mpango


 

 Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, akikabidhi zawadi ya pikipiki ya miguu mitatu mteja aliyejishindia zawadi ya pikipiki, Irene Lyamchai, kwenye shindano la 'Bonge la Mpango'. Hafla hiyo ilifanyika katika tawi la Benki ya NMB Sinza jijini Dar es Salaam. (Na Mpiga Picha Wetu).

Irene Lyamchai, akionesha kadi ya pikipiki aliyokabidhiwa baada ya kushinda  kwenye shindano la 'Bonge la Mpango'.

 

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

 

MSHINDI wa 18 wa Kampeni ya Weka Akiba na Ushinde 'Bonge la Mpango,' inayoendeshwa na Benki ya NMB, Irene Lyamchai wa Sinza, jijini Dar es Salaam, amekabidhiwa pikipiki yake ya Miguu Mitatu aina ya Lifan Cargo yenye thamani ya Sh. Mil. 4.5.

NMB Bonge la Mpango kampeni inayolenga kuhamasisha utamaduni chanya wa kuweka akiba, ilizinduliwa Februari mwaka huu na kufikia sasa imekabidhi zawadi mbalimbali zenye thamani ya Sh. Mil. 154.

Akizungumza wakati wa kumkabidhi pikipiki mshindi huyo, Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, alisema katika droo tisa zilizotangulia, jumla ya wateja 110 wamejishindia pesa taslimu, pikipiki za Miguu mitatu na gari dogo la mizigo.

"Irene Lyamchai ni mshindi wetu wa 18 kushinda pikipiki ya Miguu mitatu aina ya Lifan Cargo. Pia wamo washindi 90 waliojishindia pesa taslimu kiasi tofauti tofauti, wamo pia washindi wawili waliojibebea gari dogo la mizigo aina ya Tata Ace maarufu Kama Kirikuuu.

"Kwa ujumla washindi hao (110), wamejishindia zawadi zenye thamani ya Sh. Mil. 154, kati ya zawadi zenye thamani ya Sh. Mil. 550 zinazoshindaniwa katika Kampeni nzima ya NMB Bonge la Mpango, itakayohitimishwa kwa zawadi kuu ya gari ya kifahari aina ya Toyota Fortuner yenye thamani ya Sh. Mil. 169," alisema Donatus.

Kwa upande wake, Irene Lyamchai alikiri kuwa bahati imemuwezesha kushinda pikipiki hiyo, aliyosema itamsaidia sana katika shughuli zake za ujasiriamali na kwamba zawadi hiyo inamvika rasmi joho la ubalozi wa Benki ya NMB kwa wajasiriamali, wafanyabiashara na kwa jamii inayomzunguka.

"Nina furaha sana kwa zawadi hii ambayo sikuitegemea. Wakati nafungua akaunti NMB wala sikujua kama naweza kunufaika kwa kiwango hiki na niseme kuwa, zaidi ya kuweka akiba na kulipa wasambazaji wangu kupitia NMB, hakuna kingine kilichoniwezesha kushinda.

"Shukrani sana kwa NMB kwa hiki wanachofanya ambacho kinatutia moyo wateja wao. Zawadi hii inaenda kunisaidia sana kwenda kununulia vyakula sokoni na kufikisha eneo la biashara yangu, ambayo ilikuwa inanigharimu kiasi kikubwa cha pesa," alisema Irene.

Baada ya makabidhiano hayo, Donatus chini ya usimamizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), alichezeaha droo ya 10 ya NMB Bonge la Mpango, kusaka washindi 10 wa pesa taslimu na wawili wa pikipiki ya miguu mitatu.

Katika droo hiyo, Babyana Magori Mang'era wa Tarime mkoani Mara na Kinangwede Msuya Msuya wa Moshi mkoani Kilimanjaro, waliibuka washindi wa pikipiki mbili za Lifan Cargo, ambao watakabidhiwa katika matawi yaliyo jirani yao kwa siku na nyakati tofauti.

Washindi 10 wa pesa taslimu (kiasi tofauti) waliopatikana katika droo hiyo, majina ya matawi yao kwenye mabano ni: Rose Mbaga (Mwanjelwa), Manase Gladstone (Mandela Road),  Janeth Mlinga (Mlimani City) na Idd Shaaban (Mlimba).

Wengine walioshinda pesa taslimu ni pamoja na: Mpoki Msika (Tukuyu), Mathias Mwandelile (Kilombero), Isaya Kadunda (Chunya), Pereglino Batalingaya (Musoma), Iddy Said Salum (Kahama) na Rahel Jeremiah (Njombe).

 

 

No comments:

Post a Comment

Pages