June 01, 2021

MKUU WA MKOA MARA AFUNGUA MAADHIMISHO YA JUMA LA ELIMU KITAIFA, APONGEZA MCHANGO WA WADAU WA ELIMU

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhandisi Robert Luhumbi (katikati) akizungumza wakati alipokuwa akifungua Maadhimisho ya Juma la elimu kitaifa yanayofanyika eneo la Shirati wilayani Rorya. kulia ni Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. OcholaWayoga na Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Bw. Simon Odunga (kushoto).


Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Bw. Simon Odunga akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kwenye hafla ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Juma la elimu kitaifa yanayofanyika eneo la Shirati wilayani Rorya. 



Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. Ochola Wayoga akisisitiza jambo kwenye hafla ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Juma la elimu kitaifa yanayofanyika eneo la Shirati wilayani Rorya.


Bendi ya Shule ya Wasichana ya Kowak ikiongoza maandamano ya uzinduzi Maadhimisho ya Juma la elimu kitaifa yanayofanyika eneo la Shirati wilayani Rorya.

Baadhi ya wanafunzi kutoka shule mbalimbali za Wilaya ya Rorya wakiwa na mabango ya jumbe anuai kwenye maandamano ya uzinduzi Maadhimisho ya Juma la elimu kitaifa yanayofanyika eneo la Shirati wilayani Rorya.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhandisi Robert Luhumbi pamoja na viongozi meza kuu wakitembelea mabanda mbalimbali kwenye Maadhimisho ya Juma la elimu kitaifa yanayofanyika eneo la Shirati wilayani Rorya.  

 

Na Mwandishi Wetu, Rorya

 

MKUU wa Mkoa wa Mara, Mhandisi Robert Luhumbi amepongeza shughuli zinazofanywa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) kwa kushirikiana na Serikali kuchochea mabadiliko ya elimu kiubora nchini Tanzania. Amesema kwa kutambua mchango huo uongozi unatoa ofisi ambayo itatumiwa na wadau wa elimu mkoani hapo ili kuwasogeza karibu na kufanya kazi kwa kushirikiana zaidi.

Mhandisi Luhumbi ameyasema hayo alipokuwa akizindua Maadhimisho ya Juma la elimu kitaifa yaliyofanyika leo Wilayani Rorya, huku akikiri kuwa licha ya juhudi za Serikali katika kuboresha elimu wadau wa elimu wanaumuhimu mkubwa kushirikiana na Serikali kuboresha elimu yetu nchini.

"...Ni ukweli kwamba ili nchi yoyote iweze kundelea inahitaji kuwaelimisha wananchi wake ili wawezekupata maarifa ya kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Hivyo hapana budi ya kwamba mifumo ya elimu izingatie misingi ya usawa na iwe jumuishi. Ili hili lifanikiwe ni lazima wadau wote wawajibike kwa nafasi zao," alisema Mkuu wa Mkoa akihutubia wananchi na wadau wa elimu walioshiriki maadhimisho hayo.

Aidha aliongeza kuwa ili nchi yetu iendelee kuimarika zaidi katika uchumi wa kati hatuna budi kuwekeza nguvu zetu kwa makusudi kabisa katika elimu, na rasilimali watu wenye elimu bora ni injini ya kuleta mabadiliko chanya katika nchi. 

Hata hivyo, alisisitiza kuwa sehemu muhimu ya kuimarisha uwekezaji kwa ajili ya elimu bora ni pamoja na kuimarisha elimu msingi yaani kuanzia madarasa ya awali hadi sekondari. 

Alibainisha kuwa serikali haiwezi kwenda peke yake katika kusimamia suala hilo, bali ni lazima iunganishe nguvu ili kupata mafanikio katika elimu na mchango wa mashirika na wadau wa maendeleo unatambulika sana pamoja na wananchi.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bw. OcholaWayoga  akizungumza katika maadhimisho hayo, alisema lengo kuu la maadhimisho ni kuhamasisha juu ya malengo endelevu hasa lengo namba 4, kuhakikisha utolewaji wa elimu bora na itakaomjengea mtoto maarifa na ujuzi wa kupambana kimaisha na hasa mtoto wa kike ambaye jamii nyingi zimekuwa zikimsahau na hivyo kuishia kuolewa akiwa bado na umri mdogo.

Malengo mengine ni pamoja na kuongeza uelewa kwa umma juu ya madai ya haki ya elimu iliyo bora na kuhamasisha elimu kwa makundi maalumu kama vile watoto wenye ulemavu. Alisema miongoni mwa shughuli zitakazo fanyika baada ya ufunguzi ni kuwa na mikutano itakayofanyika vijiji mbalimbali na wananchi Juni Mosi na Pili kuwahamasisha wanajamii kushirikiana na Serikali katika kuboresha elimu iliyo jumuishi.

Hata hivyo aliongeza kuwa lengo lingine la maadhimisho hayo ni kuhamasisha jamii, Serikali na mashirika yasiyo na kiserikali umuhimu wa uwajibikaji wa pamoja katika masuala ya elimu na utekelezaji wa lengo la maendeleo endelevu la nne na hasa kuimarisha mifumo ikiwemo ya kuwekeza katika TEHAMA.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni; Uwekezaji katika mifumo ya Elimu kwa malengo ya maendeleo endelevu (Financing Education System for Sustainable Development Goals), kauli inayoikumbusha jamii umuhimu wa juhudi ya pamoja kama wadau wa elimu, yaani serikali, Asasi za Kiraia, sekta binafsi, wanafunzi, wazazi na wananchi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Pages