June 17, 2021

NMB yawaita makandarasi wakope bila dhamana



 Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB Ruth Zaipuna, (kati Kati)  akikagua reli ya kisasa(SGR) eneo la Fella Wilayani Misungwi mkoani Mwanza baada ya Rais Samia kuzindua ujenzi wa reli hiyo kilometa 341 Mwanza-lsaka (Shinyanga). Kushoto ni Afisa Mkuu wa wateja Binafsi na Biashara Filbert Mponzi na Meneja Kanda ya Ziwa NMB, Baraka Ladislaus (kulia). (Na Mpiga Picha Wetu).


Mwandishi Wetu, Mwanza


 Benki ya NMB imewaalika wakandarasi wa ndani na nje wenye mikataba ya ujenzi wa miradi ya miundombinu inayotekelezwa nchini kwenda kukopa bila kulazimika kuweka dhamana ya mikopo hiyo.


Wito huo ulitolewa jana na Afisa mtendaji mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka eneo la Fela mkoani Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga.


Alisema mikopo hiyo ni sehemu ya benki hiyo kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya ya maendeleo na malengo ya Taifa kiuchumi na kijamii.


“Tumeshirikiana na makampuni ya kigeni yanayoratibu miradi mikubwa kama ujenzi wa barabara, pamoja na miundo mbinu ya maji…mpaka sasa tumetoa dhamana ya zaidi ya Sh200 bilioni kwenye mradi wa reli ya kisasa (SGR). NMB imefanikisha zabuni kwa makandarasi wazawa zaidi ya 500 katika ngazi ya wilaya na mikoa,” alisema Zaipuna 


Afisa mtendaji mkuu huyo alisema NMB imewezesha manunuzi ya nje ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Mamlaka ya Bandari (TPA) na Bahari Kuu la Dawa (MSD) kwa kutumia Letters of Credit zenye thamani ya zaidi ya Sh120 bilioni.


“Tayari tumetoa dhamana ya Sh48 bilioni kwa kampuni za wazawa zinazotekeleza miradi ya umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini, REA,” alisema Afisa Mtendaji mkuu huyo.


Pamoja na huduma za kifedha, benki ya NMB pia inashirikiana na Serikali kupitia Shirika la Reli nchini (TRC) kulipa fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yanapitiwa na miradi ya ujenzi wa reli.


Benki hiyo pia inatekeleza kampeni ya elimu kwa umma kuhusu masuala ya kifedha kwa lengo la kupanua wigo wa ujumuishaji wa kifedha (financial inclusion) kwa makundi yote ya kijamii mijini hadi vijijini.

No comments:

Post a Comment

Pages